Thursday, August 27, 2026

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU AMPONGEZA NDEJEMBI, AMSIFIA KWA UADILIFU NA UCHAPAKAZI







Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amempongeza Mhe. Deogratius John Ndejembi kwa kuaminiwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na vyombo vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuelekea kushika dhamana ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma leo, Alhamisi, Agosti 27, 2026, wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu amesema Ndejembi amejijengea rekodi ya kuwa kiongozi mahiri, makini na mchapakazi, anayetekeleza majukumu yake kwa bidii kwa lengo la kuleta manufaa kwa Watanzania.

“Deogratius Ndejembi kama kiongozi ni kiongozi mahiri sana, ni kiongozi makini, kiongozi mchapakazi anayefanya kazi bila kuchoka ili Watanzania waweze kupata manufaa.” amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu pia amempongeza Rais Samia kwa kutambua uwezo na sifa za kiuongozi za Ndejembi, akieleza kuwa pamoja na uchapakazi wake, ana sifa za unyenyekevu, upole na utu, ambazo ni muhimu katika kubeba dhamana kubwa ya kitaifa.

Aidha, Dkt. Mwigulu amemhakikishia Ndejembi ushirikiano kutoka kwake na Mawaziri wenzake katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan katika kusimamia na kutekeleza maelekezo ya Rais Samia yanayolenga kuendeleza ujenzi wa Tanzania.

Kauli hiyo inaonesha imani katika uwezo, uzoefu na sifa za kiuongozi za Ndejembi, huku ikisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano wa viongozi katika kuendeleza utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

No comments:

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU AMPONGEZA NDEJEMBI, AMSIFIA KWA UADILIFU NA UCHAPAKAZI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba , amempongeza Mhe. Deogratius John Ndejembi kwa kuaminiwa ...