
Tanzania na China zinatarajia kufungua sura mpya ya ushirikiano katika usimamizi na maendeleo ya mashirika ya umma, kupitia makubaliano yatakayoweka msingi wa kubadilishana uzoefu, utaalamu na kujenga uwezo wa taasisi za Serikali.
Hatua hiyo inakuja wakati Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha hati mbili za makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Tume ya Usimamizi wa Mali za Serikali za China (SASAC) pamoja na Jumuiya ya China ya Mageuzi na Maendeleo ya Mashirika (CERDS).
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Jumatano Agosti 26, 2026, wakati wa mkutano na ujumbe wa wataalamu kutoka China, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema makubaliano hayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Ijumaa au Jumatatu ijayo.
Mchechu alisema ushirikiano huo utafungua fursa kwa taasisi za umma za Tanzania na China kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo ya utafiti, kujenga uwezo wa taasisi, sera, utawala bora, mageuzi ya mashirika ya umma na tathmini ya utendaji.
Aidha, Tanzania inatarajia kutumia ushirikiano huo kujifunza kutokana na uzoefu wa China katika usimamizi wa mali za Serikali, uendeshaji wa mashirika ya umma kwa kuzingatia misingi ya soko na namna ya kuongeza ufanisi na thamani ya mtaji wa Serikali.
“Kupitia uhusiano wetu wa pande mbili na SASAC, tunalenga kujifunza namna China ilivyofanikiwa kufanya mageuzi na kuelekeza mtaji wa Serikali katika sekta muhimu za kimkakati ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Mchechu.
Kwa sasa, OTR inasimamia taasisi za umma 308, zikiwamo 252 ambazo Serikali inamiliki hisa nyingi na 56 ambazo Serikali ina hisa chache.
Kwa upande wake, Rais wa CERDS, Peng Huagang, alisema uzoefu wa China umeonesha kuwa mashirika ya umma yanaweza kuendeshwa kwa misingi ya soko na ushindani huku yakiendelea kutekeleza majukumu yake ya kimkakati kwa taifa.
Alisema mageuzi hayo yanalenga kujenga mashirika yaliyo imara zaidi, yenye ufanisi na uwezo wa kushindana, sambamba na kuhakikisha mali na mitaji ya Serikali inalindwa na kuongezeka thamani.
“Mageuzi yanayozingatia misingi ya soko ndiyo njia ya msingi ya kuongeza ushindani wa mashirika ya umma, na kuyawezesha kufanya kazi kwa ufanisi sambamba na aina nyingine za umiliki,” alisema Peng.
Alisema ushirikiano huo pia unaendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China na unaendana na utekelezaji wa ahadi zilizowekwa kupitia Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
FURSA ZA USHIRIKIANO
Sura hiyo mpya ya ushirikiano pia inatarajiwa kufungua fursa katika sekta za kimkakati, ikiwamo miundombinu, reli, bandari, usafiri wa anga, uhandisi, teknolojia, viwanda na usafirishaji wa mizigo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Dkt. Boniphace Nobeji, alisema uboreshaji wa utendaji na ufanisi wa bandari una nafasi kubwa katika kukuza biashara na maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Tunaamini ustawi wa taifa lolote unatokana na biashara, na sehemu kubwa ya biashara inawezeshwa na bandari zenye ufanisi. Hakuna shaka kwamba maboresho katika utendaji na ufanisi wa TPA yataharakisha maendeleo ya kiuchumi ya Afrika Mashariki na Kati,” alisema Dkt. Nobeji.
Alitaja maeneo yanayoweza kunufaika na ushirikiano huo kuwa ni pamoja na uendelezaji wa bandari kavu, uhamishaji wa teknolojia, ujenzi wa uwezo na kujifunza kutokana na uzoefu wa China katika usimamizi wa bandari.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, alitaja fursa katika vituo vya usafirishaji wa mizigo, huduma za usafirishaji wa mizigo, kongani za viwanda zinazounganishwa na reli pamoja na vituo shirikishi vya usafirishaji.
Pia alibainisha uwezekano wa kutumia mfumo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) katika ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kando ya korido za reli.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), John Nzunda, alitaja usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga, matengenezo na uhandisi, teknolojia za kidijitali, usimamizi wa mafuta na mafunzo maalumu kwa wataalamu wa sekta ya anga kuwa miongoni mwa maeneo yenye nafasi ya kuimarishwa kupitia ushirikiano huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CCECC East Africa Ltd, Lu Haiqiang, alisema kampuni hiyo iko tayari kuimarisha ushirikiano na mashirika ya umma ya Tanzania katika maeneo ya miundombinu, uhandisi, ujenzi na uendeshaji.
Alitaja pia ufufuaji wa Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) kuwa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa kuunganisha korido za biashara na shughuli za madini, kilimo, usafirishaji na viwanda.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi na wataalamu kutoka OTR, SASAC na CERDS, Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, pamoja na viongozi waandamizi kutoka TPA, TRC na ATCL, ukiweka msingi wa hatua mpya ya ushirikiano kati ya mashirika ya umma ya Tanzania na China.
.jpeg)

No comments:
Post a Comment