Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo na kuwaaga wanafunzi walionufaika na Samia Scholarship Extended wanaokwenda kuendelea na masomo nchini Ireland na Urusi, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Agosti 28, 2026.
Wanafunzi hao watapata fursa ya kujiendeleza katika maeneo ya kimkakati ya Sayansi ya Data, Akili Unde (Artificial Intelligence) na Sayansi Shirikishi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuwekeza katika maarifa, teknolojia na rasilimali watu yenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa na yajayo.
Mazungumzo ya Mhe. Rais na wanafunzi hao yamebeba ujumbe wa matumaini na dhamira ya Tanzania ya kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika medani za kimataifa, huku wakitarajiwa kurejesha maarifa na ujuzi watakaoupata kwa manufaa ya Taifa.
Kupitia Samia Scholarship Extended, Serikali inaendelea kufungua milango ya elimu ya kiwango cha juu kwa vijana wa Kitanzania na kuandaa kizazi cha wataalamu kitakachochangia katika mageuzi ya kidijitali, ubunifu na maendeleo endelevu ya Taifa.
Safari yao kwenda Ireland na Urusi si safari ya elimu pekee, bali ni uwekezaji katika mustakabali wa Tanzania.














No comments:
Post a Comment