TANGA, 01 Machi 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekamilisha ziara yake ya kikazi mkoani Tanga kwa kutembelea na kukagua maboresho ya gati mbili mpya katika Bandari ya Tanga.
Baada ya ukaguzi huo, Rais amezungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo, akisisitiza umuhimu wa maboresho hayo katika kukuza uchumi wa taifa na kuimarisha biashara ya kimataifa kupitia bandari za Tanzania.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais ameeleza kuwa maboresho ya gati hizo mbili yamefanyika ili kuongeza ufanisi wa bandari na kuhakikisha inakidhi mahitaji ya wateja wa ndani na nje ya nchi. Amebainisha kuwa hatua hii ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya bandari ili kuvutia wawekezaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika sekta ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari.
"Maboresho haya tunayoyafanya katika Bandari ya Tanga ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari ili kuhakikisha tunapunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma," alisema Rais Samia.
Rais alitoa pongezi kwa wafanyakazi wa bandari hiyo kwa juhudi zao katika kuhakikisha bandari inazidi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Aidha, aliwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na kuzingatia maadili ya kazi ili kuleta tija zaidi kwa taifa.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa bandari, ikiwa ni pamoja na kuongeza vitendea kazi vya kisasa na kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kukidhi mahitaji ya sekta hiyo inayobadilika kwa kasi.
Katika ziara hiyo, Rais aliambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pamoja na viongozi wa Mkoa wa Tanga. Viongozi hao walimweleza Rais kuwa maboresho hayo yameanza kuleta matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya meli zinazotia nanga bandarini hapo, hivyo kuimarisha biashara na uchumi wa mkoa huo.
Wananchi wa Tanga, hususan wafanyakazi wa bandari, walionesha shukrani zao kwa Rais kwa maboresho hayo, wakiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Ziara ya Rais Samia katika mkoa wa Tanga imehitimishwa kwa mafanikio, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada zake za kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji inaboreshwa ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment