Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 20, 2025) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mitambo ya kuzalisha oksijeni kwa matumizi ya hospitali, ambapo amesisitiza kuwa soko linatakiwa liwe na bidhaa salama, bora, na zinazokubalika kimataifa. Mitambo hiyo inajengwa katika ofisi za TOL Gases, Temeke Dar es Salaam.
Amesema mradi huo utakapokamilika utazalisha lita milioni 4.1 za oksijeni ya matibabu kwa mwaka kuanzia mwaka 2026. “Hatua hii itaboresha upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na vituo vya afya, pamoja na kupunguza gharama za oksijeni ya matibabu kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya kote nchini, hivyo kuimarisha huduma za afya kwa wananchi”.
Aidha, Waziri Mkuu amesema mradi huu unaunga mkono juhudi endelevu za Serikali za kuhakikisha oksijeni kwa ajili ya matibabu inapatikana kwa urahisi katika kila kituo cha huduma za afya nchini.
“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na zahanati nchini na kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya kupumua ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na kuokoa ya watoto wa Taifa hili.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godfrey Mollel amesema mradi huo ni muhimu kwa sababu oksijeni inayozalishwa kwa njia hiyo inakuwa na viwango vya ubora, hivyo itasaidia kuimarisha huduma za afya zitolewazo nchini pamoja na kupunguza vifo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Daniel Warungu ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujidhatiti katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.
Amesema kampuni ya TOL inajivunia kushirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya kuboresha huduma za afya, hususani upatikanaji na usambazaji wa gesi ya oksijeni kwa ajili ya matibabu ukiwemo mradi wa shilingi bilioni 9.8 wa ufungaji wa mifumo ya usambazaji gesi wodini katika vituo 129 vya huduma za afya nchini kote
No comments:
Post a Comment