Mataka apandishwa kizimbani




MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kuweka kumbukumbu za manunuzi ya magari chakavu yenye thamani ya zaidi ya Sh 1 bilioni.

Mbali ya Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Elisaph Ikomba ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa shirika hilo na William Haji ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa mahesabu wa shirika hilo.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincon alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo kati ya Juni na Julai 2007.

Katika shitaka la kwanza ambalo linawahusu washtakiwa wote, ilidaiwa kuwa kati ya Juni na Julai 2007 Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa nafasi zao walishindwa kutunza kumbukumbu za taarifa za kukubali zabuni ya ununuzi wa magari chakavu 26.

Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa shtaka la pili nalo linawahusu washtakiwa wote ambapo inadaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 washtakiwa kwa pamoja walishindwa kufuata taratibu za manunuzi ya umma katika ununuzi wa magari chakavu 26 yenye thamani ya Dola za Marekani 809,300,000 kutoka katika kampuni ya Bin Dalmouk Morots Co. Ltd ya nchini Dubai.

Katika shtaka la tatu linalomuhusu Mattaka, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 mshtakiwa akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa ATCL alitumia madaraka yake vibaya katika ununuzi wa magari hayo bila kuwepo kwa mkataba wa zabuni uliosainiwa na pande zote mbili na kuhakikiwa na bodi ya zabuni ya shirika hilo suala ambalo ni kinyume cha sheria.

Comments

Anonymous said…
I natakiwa sheria iwe msumeno.Watu wa kashfa ya rada pia washtakiwe lakini Takururu inaogopa kwa nini?Tusubiri mpaka nchi ije iwe kama Libya?Hatuwezi kupata msaada wowote wa kubadili nchi iwe ya haki kwani hatuna mafuta ni masikini kazi ni kwetu sisi wenyewe watanzania