Vodacom yatangaza zawadi za Mwanza Cycle Challenge



Vodacom Tanzania imetangaza zawadi zitakazotolewa kwa washindi mbalimbali watakaoshiriki mashindano ya baiskeli ambayo yatafanyika Jijini Mwanza mwezi huu yanayotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 50.

Akizungumza naWaandishi wa Habari, Jijini leo, katika makao makuu ya Vodacom Tanzania yaliyopo Mlimani City Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Rukia Mtingwa alisema kwamba mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na kuwaomba waendesha baiskeli kujitokeza kwa wingi.

“Mashindano haya yameboreshwa kwa upande wa zawadi, ubora na viwango,” alisema.

Aidha alifafanua kuwa mashindano hayo yatafanyika kwa siku mbili yaani Novemba 12 na 13 mwezi huu na kwamba tarehe 12 itakuwa maalumu kwa mashindano ya walemavu ambao watashindana kilometa 15 kwa wanaume na 10 kwa wanawake. Na tarehe 13 Novemba yatafanyika mashindano ya kilomita 196 kwa wanaume, 80 kwa wanawake ambapo kwa upande wa walemavu ni Kilometa 15 kwa walemavu wanaume na Kilomita 10 kwa walemavu wanawake.

Akitangaza zawadi hizo kwa washiriki wa mbio za kilometa 150 Mtingwa alisema mshindi wa kwanza atajipatia shilingi 1,500,000, wa pili kiasi cha 1,000,000, wa tatu 700,000, ambapo mshindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atajipatia shilingi 500,000 kila mmoja. Aidha kwa upande washindi wa 11 hadi 20 kila mmoja atajinyakulia kitita cha 250,000 kila mmoja, na kuanzia mshindi wa 21 hadi wa 30 watapatia shilingi 90,000 kila mmoja.

Kwa upande wa mbio za mita 80 kwa wanawake mshindi wa kwanza pia atajipatia zawadi ya shilingi milioni 1,100,000, wa pili 800,000, mshindi wa tatu 600,000, wakati washindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atazawadia kiasi cha shilingi 350,000 kila mmoja. Vilevile washindi watakaoshika nafasi ya 11 hadi ya 20 katika mbio hizo watapewa jumla ya 130,000 kila mmoja, na kuanzia mshindi wa 21 hadi wa 30 watapatia shilingi 70,000 kila mmoja.

Mbali na hayo Mtingwa alibainisha kwamba kwa upande wa mbio za kilometa 10 ambazo zitawashirikisha watu wenye ulemavu alisema washindi wa kwanza wawili kila mmoja atajipatia jumla ya shilingi 400,000.

Kwa washindi wa pili wawili nao watajishindia kiasi cha shilingi 250,000 kila mmoja, washindi wa tatu wawili kila mmoja atapewa kiasi cha 150,000 kila mmoja wakati washindi wa nne wane hadi wa kumi watajipatia kitita cha 70,000 kila mmoja.

Comments