Mwenyekiti wa kamati ya uangalizi wa uchaguzi ya chuo kikuu cha Dar es Salaam (TEMCO) Profesa Rwekaza Mukandala akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya awali ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambapo ripoti hiyo inaeleza kuwepo kwa mapungufu kwa baadhi ya maeneo ingawa inaeleza ulikuwa huru, kulia ni makamu mwenyekiti Temco Maryam Abubakar. Picha na Said Powa
*********************************************************************************
TIMU ya Waangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu (Temco) imetoa tathmini yake ya awali kuhusu uchaguzi huo uliofanyika Oktoba31, ikionyesha kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya walikisaidia chama tawala katika kampeni zake.
Temco pia imeonyesha kuwepo kwa dalili za kuvunjwa kwa sheria ya gharama za uchaguzi kutokana na baadhi ya vyama kutoa mabango mengi na vifaa vingine vya kampeni hizo vyenye gharama kubwa.
Katika taarifa yake hiyo ya awali mbele ya wanahabari jana Temco kupitia mkwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala imetaja kuwepo kwa vitendo vilivyotishia uvunjifu wa amani na vurugu ikibainisha kuwa vyama vya CCM, Chadema na Cuf kuhusika.
“Mambo yasiyofaa yaliyobainishwa na timu ya waangalizi wa Temco si mageni, lakini yameonekana kuchukua nafasi kubwa katika uchaguzi wa mwaka huu,”alisema Profesa Mukandala na kufafanua:
Wakuu wa mikoa na wilaya walitumia rasilimali za taifa kama magari katika kampeni za urais kumsaidia mgombea anayetetea nafasi yake.”
Mwenyekiti huyo wa Temco aliongeza kuwa mara kadhaa katika kampeni zake mgombea urais huyo alitumia nafasi yake kama kiongozi wa nchi kutoa au kubadili uamuzi wa serikali kama ahadi kwa wapiga kura ili kujipatia wapiga kura jambo ambalo wagombea wengine hawakuweza kulifanya.
Temko ilitembelea majimbo 135 kati ya 223 ikiacha majimbo ya uchaguzi ambayo wagombea wake walipita bila kupingwa na kutoa alama A mpaka E kwa majimbo.
Mukandala alisema kuwa mgombea kutoa ahadi si jambo baya lakini kutoa ahadi au uamuzi kutumia madaraka aliyonayo mtu ili kuvuna wapiga kura syo jambo sahihi.
Wakati wa kampeni za kuwania urais, ubunge na udiwani kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita, vyama vya upinzani vililalamikia baadhi ya wagombea nafasi hizo kutumia nyadhifa zao kutoa ahadi kwa lengo la kuvuna wapigakura.
Akizungumzia uvunjaji sheria ya gharama za uchaguzi, mwenyekiti huyo wa Temco alisema kuwa, “Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kwanza kufanyika chini ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi uliolenga kudhibiti matumizi makubwa ya fedha, lakini kumekuwepo na vifaa vingi vya gharama kubwa kwa vyama vikubwa hasa chama tawala CCM.”...
Imeandikwa na Exuper Kachenje: SOURCE: MWANANCHI
Comments