Thursday, November 20, 2025
Wednesday, November 19, 2025
SADC Yazindua Mkakati wa Mawasiliano wa mwaka 2025-2030
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezindua Mkakati wa Mawasiliano na Uhamasishaji wa Mwaka 2025-2030 ili kuimarisha mawasiliano, uhusiano wa kikanda na maendeleo endelevu, kwa nchi wanachama.
Hafla ya Uzinduzi wa Mkakati huo imefanyika tarehe 17 Novemba, 2025 jijini Gaborone, Botswana na kushirikisha wadau mbalimbali wa mawasiliano, habari na washirika wa kimataifa wa maendeleo.
Akizindua mkakati huo, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda Bi. Angele Makombo Ntumba amesema mkakati huo utasaidia kukuza mfumo wa mawasiliano katika karne hii ya kidigitali na kuwezesha ukanda wa Afrika ya Kusini kuimarisha miundombinu, uchumi, biashara na miradi ya maendeleo ya jamii, kwa manufaa ya nchi wanachama.
Bi. Ntuma amesema Mkakati huo wa Mawasiliano
uliozinduliwa katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno, utatekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa SADC chini ya Waratibu wa Kitaifa wa SADC na Waratibu wa Kitaifa wa Habari na Mawasiliano wa jumuiya hiyo, katika nchi wanachama 16 za SADC.
Amewataka waratibu hao kushirikiana na SADC na wadau mbalimbali katika kutekeleza Mkakati huo, wakiwemo Vyombo vya Habari na Taasisi za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika nchi zao na ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Aidha, Bi. Ntumba ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo la GIZ kwa kudhamini maandalizi na uzinduzi wa mkakati huo, kwani umewezesha SADC kutekeleza majukumu yake kwa upana zaidi kupitia nyenzo muhimu ya Mawasiliano na Uhamasishaji.
Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini Botswana, Bi. Simone Goertz ameelezea azma ya GIZ kuendeleza ushirikiano na SADC katika utekelezaji wa Mkakati wake Mawasiliano, hatimaye kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya nchi wanachama; kulingana na mabadiliko ya utandawazi yanayoendelea kutokea duniani.
Sunday, November 16, 2025
KAMISHNA WA UHIFADHI TANAPA AFANYA ZIARA YA KIKAZI KITUO CHA MALIKALE – MTWA MKWAWA, IHINGA, IRINGA
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, amefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Malikale cha Makumbusho ya Mtwa Mkwawa, kilichopo Kalenga, mkoani Iringa, ikiwa sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kukagua na kuimarisha utendaji katika vituo mbalimbali vya urithi wa taifa.
Akiwa katika ziara hiyo, Kamishna Kuji alipata fursa ya kukutana na familia ya Mtwa Mkwawa inayoongozwa na Mtwa Abdu Adam Sapi Mkwawa – Mfwimi II, Chifu wa sita wa ukoo wa Mtwa Mkwawa (Kabila la Wahehe).
Mazungumzo yao yalijikita katika njia bora za kuimarisha usimamizi wa Makumbusho ya Mtwa Mkwawa, kuendeleza mahusiano na jamii inayouzunguka, pamoja na kuhakikisha historia, tamaduni na asili ya kabila la Wahehe zinaendelea kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kamishna Kuji ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya TANAPA, viongozi wa ukoo pamoja na jamii, ili kuhakikisha kituo hicho muhimu cha kihistoria kinaendelea kuwa rejea na fahari ya utamaduni wa Mtanzania.
#tanapaupdates #MtwaMkwawaMuseum #MalikalezaTANAPA #TanzaniaParks #tumerithishwatuwarithishe
Friday, November 14, 2025
RAIS DKT. SAMIA AMUAPISHA DKT. MWIGULU KUWA WAZIRI MKUU WA TANZANIA
Katika hafla yenye utofauti, heshima na hamasa mpya kwa Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 14, 2025, amemuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, pamoja na wananchi waliojitokeza kushuhudia hatua hiyo muhimu katika uongozi wa nchi.
Dkt. Mwigulu, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini, ametajwa kuwa miongoni mwa viongozi wenye rekodi ya utendaji, uthabiti wa uongozi na uwezo wa kusimamia mageuzi ya kiuchumi na kijamii. Uteuzi wake unaangaliwa kama mwanzo mpya wa msukumo wa kasi katika utekelezaji wa agenda za maendeleo zinazolenga kuinua maisha ya Watanzania.
Rais Dkt. Samia alisisitiza umuhimu wa uadilifu, uwajibikaji na kasi ya utendaji katika kuwatumikia wananchi, huku akimtaka Waziri Mkuu mpya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuimarisha uchumi na kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia wananchi kwa ufanisi na usawa.
Wananchi na wadau mbalimbali nchini wamepokea tukio hilo kwa matumaini mapya, wakiona uteuzi huo kama chachu ya kuimarisha mwelekeo wa Taifa katika ujenzi wa uchumi shindani, Serikali shirikishi na maendeleo endelevu.
Thursday, November 13, 2025
MIRADI YA CSR YA MIGODI YAWANUFAISHA WANANCHI SIMIYU
Serikali imesema itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa na kampuni za uchimbaji madini nchini, ili kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na migodi wananufaika moja kwa moja na shughuli za uchimbaji madini.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela, alisema hayo hivi karibuni alipokagua utekelezaji wa miradi ya CSR inayofanywa na kampuni za uchimbaji madini katika mkoa huo, akibainisha kuwa miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya umeme.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi. Ndiyo maana tunasisitiza kampuni zote za uchimbaji, zikiwemo zinazomilikiwa na wachimbaji wadogo, kutekeleza wajibu wao wa kijamii kupitia miradi ya CSR ili jamii inayoishi jirani na migodi inufaike moja kwa moja na rasilimali hizo,” alisema Makolobela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya EMJ Mining iliyopo eneo la Dutwa mkoani Simiyu, Masanga Silanga, alisema kampuni hiyo inajihusisha na uchimbaji wa dhahabu kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka China, jambo lililoongeza ufanisi na teknolojia katika shughuli zao za uchimbaji.
Alisema kampuni hiyo huzalisha wastani wa kilo 10 za dhahabu kwa mwezi endapo kuna upatikanaji mzuri wa mwamba wenye madini (mbale), ingawa wakati mwingine hukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa mwamba kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na mishororo midogo ya dhahabu (narrow vein).
Silanga alibainisha kuwa kampuni yake imetekeleza miradi kadhaa ya CSR ikiwemo kutoa madawati 50 na matofali 2,000 kwa Shule ya Msingi Dutwa, mashine za kuchapisha (printer) na nakala (photocopy) kwa taasisi za elimu, pamoja na mchango wa matofali 2,000 kwa Hospitali ya Nguno.
“Tayari tumewekeza zaidi ya Dola 50,000 katika miradi ya CSR, ikiwemo mradi wa kuvuta umeme kutoka Dutwa hadi vijiji vya jirani ambavyo awali havikuwa na huduma ya umeme,” alisema Silanga.
Naye Meneja wa Mgodi huo, Noah Wang, alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa ni upungufu wa mwamba wenye madini (mbale), hali inayosababisha baadhi ya mitambo kusimama na kupunguza uzalishaji.
“Mitambo yetu ina uwezo wa kuchakata hadi tani 500 za mwamba kwa siku, lakini kwa sasa hatupati kiwango hicho, jambo linalolazimisha baadhi ya mitambo kuzimwa mara kwa mara. Kwa sasa shaft moja pekee ndiyo inaendelea na kazi, hivyo uzalishaji umeshuka kwa kiasi kikubwa,” alisema Wang.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imeajiri jumla ya wafanyakazi 48, wakiwemo 30 wazawa na 18 raia wa China, wanaofanya kazi kwa mfumo wa kupokezana (shift system).
Wednesday, November 12, 2025
Wachimbaji Wadogo wa Madini Simiyu Wapaza Sauti: “Tunaweza Tukipewa Umeme na Mikopo
WACHIMBAJI Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Simiyu wameiomba Serikali pamoja na taasisi za kifedha kuwaunga mkono kwa kuwapatia umeme wa kudumu na mikopo yenye masharti nafuu, wakisema changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa katika kuongeza uzalishaji wa madini, hususan dhahabu.
Mmoja wa wachimbaji wanawake kupitia Chama cha Wachimba Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) mkoani humo, Anisia Japhet, amesema wamekuwa wakitumia gharama kubwa kuendesha mitambo kutokana na kutegemea nishati ya dizeli.
“Tunatumia dizeli ambayo ni ghali. Lita 80 zinamalizika ndani ya saa 24. Tungepata umeme wa kudumu, tungepunguza gharama na kuongeza tija,” amesema Anisia.
Ameongeza kuwa uchimbaji si kazi ya wanaume pekee bali ni fursa yenye manufaa makubwa kwa wanawake wanaojituma.
“Nikiwa mwanamke, nimefanikiwa kusomesha watoto na kuendesha maisha yangu kupitia uchimbaji. Kila mwezi tunapata wastani wa viroba 100 vya mawe, na kila kiroba kinaweza kutoa gramu moja au zaidi za dhahabu,” ameongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi wa TAWOMA, Paul Ntalima, amesema wanamiliki maduara 24 ya uzalishaji, lakini ni maduara 14 pekee yanayoendelea na kazi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
“Wachimbaji wadogo wana uwezo wa kuongeza tija mara mbili zaidi endapo watapatiwa mikopo yenye riba nafuu. Tunatengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya 400. Sekta hii si tu inaleta kipato, bali pia inaimarisha maisha ya wananchi. Tukipata umeme wa gridi, uzalishaji utaongezeka mara mbili hadi tatu,” amesema Ntalima.
Naye Mussa Kazidishi, Mtendaji wa Mgodi wa Ludovic Mlalo & Partners, amesema mgodi wao unaajiri zaidi ya wafanyakazi 200 na umeendelea kurejesha kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.
“Jamii inanufaika hasa wakati wa mvua ambapo barabara huboreshwa na milipuko ya magonjwa hupungua. Tukipatiwa mikopo ya riba nafuu na nishati ya kudumu ya umeme, uzalishaji wetu utaongezeka mara tatu,” amesema Kazidijshi.
Akizungumzia changamoto hizo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela, amesema Serikali kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na TANESCO inaendelea na mazungumzo kuhakikisha maeneo yote ya wachimbaji wadogo mkoani humo yanapatiwa umeme wa kudumu.
“TANESCO wameahidi kufikisha umeme katika maeneo yote ya wachimbaji wadogo mkoani Simiyu ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema Makolobela.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kufanya tafiti zaidi katika maeneo ya madini ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya uchimbaji wenye tija.
“Wito wangu kwa taasisi za kifedha ni kuangalia upya namna ya kuwakopesha wachimbaji wadogo, kwa kuwa wana bidhaa halisi, masoko yapo, na taarifa zao za kifedha zinajulikana. Wana uwezo wa kurejesha mikopo,” amesisitiza Makolobela.
Amebainisha kuwa kwa sasa Mkoa wa Simiyu una vituo vitano vya ununuzi wa madini na soko kuu moja lililopo Bariadi Mjini, ambako shughuli kubwa za biashara ya madini hufanyika.
Makolobela pia amewapongeza wachimbaji kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), akitaja mfano wa vikundi vya TAWOMA na EMJ vilivyotoa zaidi ya madawati 90 kwa Shule ya Majengo kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.
Friday, November 07, 2025
đź”´đź”´HIFADHI YA MPANGA-KIPENGERE YAENDELEA KUWA LULU YA VIZAZI VIJAVYO
📍Wanafunzi wa Nyanda za Juu Kusini Wapiga Kambi Kujifunza na Kutali
Na Beatus Maganja, Njombe.
Wahenga walioshiba tunu za uhifadhi na utalii nchini waliwahi kusema "Kama unataka kujua uzuri wa Tanzania tembea ndani ya moyo wake, na moyo huo ni Hifadhi zake". Wengine walisema "Kuna safari ambazo hubadilisha mawazo, na kuna nyingine zinazogusa mwili, nafsi, moyo na roho".
Kuna mahali duniani ambapo miamba huzungumza Kwa sauti ya utulivu, mito ikiimba nyimbo za kale na upepo ukiandika mashairi yasiyofutika juu ya majani ya kijani, mahali ambapo asili huvaa vazi za kizalendo, mahali ambapo historia ikiishi, elimu ikitembea na Tanzania ikitabasamu. Hapa ndipo unapoikuta Hifadhi ya Mpanga-Kipengere, hifadhi iliyopo Mikoa ya Mbeya na Njombe ikiwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA.
Leo Novemba 7, 2025 TAWA tulishuhudia ukurasa mwingine mzuri wa historia ya elimu na uhifadhi ulioandikwa ndani ya Hifadhi hii, wakati walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lupalilo kutoka Mkoa wa Njombe walipoitembelea Kwa ziara ya kujifunza na kutalii.
Ziara hii si safari ya kawaida, bali mwendelezo wa hamasa inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TAWA inayosisitiza dhana ya "Tumerithishwa Tuwarithishe" lakini pia dhana ya "Tembea Tanzania, Jifunze Tanzania" dhana za utalii wa ndani zilizovuka mipaka ya starehe na kuwa chombo cha elimu, uchumi na uzalendo.
Kwa miaka kadhaa sasa, Shule ya Lupalilo imekuwa mfano wa Kuigwa Kwa kuleta wanafunzi Mpanga-Kipengere, Si Kwa kutazama tu mandhari yake, bali kujifunza Kwa macho, miguu na akili. Mahali ambapo kila mwamba ni somo, kila korongo ni darasa na kila chemichemi ni nukuu ya uumbaji.
Ni Hifadhi pekee nchini ambapo mwanafunzi huweza kushuhudia miamba yote mitatu ya sayansi ya jiolojia. Mwamba moto, mwamba tabaka na mwamba geu.
Lakini Mpanga-Kipengere haizungumzi tu jiolojia, bali ni kitovu cha urithi wa historia ya Tanzania, mahali ambapo bado yanapumua majina makubwa ya Chifu Mkwawa Mkwavinyika na Chifu Merere, mashujaa waliotetea ardhi hii kabla haijawa hifadhi wakiamini kuwa nchi bila heshima ya ardhi yake ni nyumba isiyo na msingi.
Kupitia ziara kama hizi, vijana wanajengewa moyo wa uzalendo, kupenda mazingira na kuthamini rasilimali za taifa. Ni mahali ambapo vizazi vinalelewa si tu kuwa wasomi, bali walinzi wa urithi wa Tanzania.
Kwa maneno mafupi, Hifadhi ya Mpanga-Kipengere ni darasa liliandikwa Kwa mikono ya Muumba mwenyewe, ni darasa la uhai,mahali ambapo kila mgeni huondoka na zawadi inayoonekana Kwa macho ya nyama, zawadi ya kutua msongo wa mawazo na kuongeza upendo Kwa nchi yake, mahali ambapo mgeni huondoka akiwa amebeba zaidi ya kumbukumbu na ndoto mpya, ndoto ya kizazi kinachotambua kuwa utalii ni darasa, na uhifadhi ni urithi.
Karibu Hifadhi ya Mpanga-Kipengere, Hifadhi hii ni salama na atakaye aje
Waziri Mkuu azindua boti mbili za doria na uokozi
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa siku 14 kwa wizara na taasisi zinazohusika na Kituo cha Kitaifa cha pamoja cha Oparesheni zipeleke w...
-
Hapa mmoja wa watoto hao akiwa na kijana mwenzake mwenye miaka 18, wote wako sawa lakini yeye hawezi kuzungumza kama watu wa kawaida. Mama S...
-
Nadhani mtakumbuka kibwagizo maarufu katika TV ambacho kinaimbwa perupe pepero perupe pepero hawa ni vijana wa Sisi Tambala waliokuwapo kati...
-
Mdau Julius Samwel hivi karibuni alikuwa huko Mwanza na hizi ndizo alizofanikiwa kutumegea, wadau hebu someni hicho kibao mniambie kuna nini...






.jpeg)


.jpeg)





.jpeg)
.jpeg)


















.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)