Na OWM – TAMISEMI, Lushoto
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza Kituo cha Elimu ya Kiislamu Irshaad (Irshaad Islamic Centre) kilichopo Lushoto, Mkoa wa Tanga, kufuatia ombi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Lushoto na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe.
Msaada huo utasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kituo hicho, ikiwemo kuboresha Chuo cha Ufundi, kujenga madrasa ya kisasa, nyumba za walimu, hospitali, ukumbi wa mikutano, jengo la wageni pamoja na bustani ya kisasa, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa elimu na huduma za kijamii kwa wananchi wa Lushoto na maeneo jirani.
Prof. Shemdoe aliwasilisha ombi hilo wakati wa Sherehe ya Maulidi ya Kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W.) zilizofanyika Julai 5, 2026 katika Kituo cha Irshaad Islamic Centre, ambapo Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi alikuwa Mgeni Rasmi.
Katika tukio hilo, Rais Mwinyi pia alikubali ombi la Sheikh Sharrif Hussein Ahmad Badawiyy la kuwa Mlezi wa Kituo cha Irshaad Islamic Centre, akiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi na wadau mbalimbali katika kukiendeleza ili kiwe kitovu cha elimu bora, maadili mema na maendeleo ya jamii.
Aidha, Rais Mwinyi aliridhia ombi la kutambua mchango wa Hayati Alhaji Ali Hassan Mwinyi kwa kuruhusu bustani itakayojengwa ndani ya Chuo cha Ufundi cha kituo hicho kuitwa jina lake, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taasisi hiyo.
Wito wa Prof. Shemdoe uliungwa mkono na viongozi mbalimbali waliochangia kwa hiari yao, akiwemo yeye mwenyewe aliyetoa Shilingi Milioni 20, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Burian (Milioni 5), Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (Milioni 5), Mbunge wa Bumbuli Mhandisi Ramadhani Hamza (Milioni 5), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Bw. Rajab Abdallah (Milioni 3) na Mbunge wa Afrika Mashariki Dkt. Abdullah Makame (Milioni 5), na kufanya jumla ya michango kufikia Shilingi Milioni 248.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Prof. Shemdoe alimshukuru Rais Mwinyi kwa kukubali ombi hilo, akieleza kuwa msaada huo utakuwa chachu ya kuimarisha elimu, kukuza ustawi wa jamii na kuboresha huduma zinazotolewa na Kituo cha Irshaad.
Wananchi na viongozi waliohudhuria hafla hiyo walimpongeza Rais Mwinyi kwa uamuzi huo, wakieleza kuwa utaacha alama ya kudumu katika maendeleo ya elimu, ujuzi na huduma za kijamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo katika Wilaya ya Lushoto.











No comments:
Post a Comment