Arusha: Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Klabu ya Simba Sports Club zimeanzisha ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuitangaza Tanzania kupitia utalii na michezo, hatua inayotarajiwa kuongeza hamasa ya kutembelea vivutio vya utalii nchini huku ikiimarisha taswira ya Tanzania kimataifa.
Akizungumza katika uzinduzi wa ushirikiano huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA, Dkt. Harrieth Mtae, alisema ushirikiano huo ni mwanzo wa enzi mpya unaoonyesha namna sekta ya umma na taasisi za michezo zinavyoweza kushirikiana kuleta thamani kwa taifa.
"Ninawashukuru viongozi wa Simba Sports Club kwa kukubali kuwa washirika wetu katika safari hii muhimu ya kuitangaza Tanzania kupitia michezo na utalii. Leo tunashuhudia mwanzo mpya wa ushirikiano unaounganisha chapa mbili kubwa za Afrika kwa lengo la kuitangaza Tanzania duniani," alisema Dkt. Mtae.
Alieleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA inaunga mkono kikamilifu ushirikiano huo kwa kuwa unaendana na maono ya kuifanya Ngorongoro kuwa kivutio cha utalii cha kiwango cha kimataifa, sambamba na kuchangia utekelezaji wa vipaumbele vya taifa katika kukuza utalii, uchumi na diplomasia ya kimkakati.
Kwa mujibu wa Dkt. Mtae, kupitia kampeni ya "The Pride Returns Home", mamilioni ya Watanzania pamoja na mashabiki wa mpira wa miguu ndani na nje ya nchi watapata sababu mpya ya kutembelea Ngorongoro na kujivunia urithi wa kipekee wa Tanzania.
Alibainisha kuwa wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za AFCON 2027, ushirikiano huo unathibitisha kuwa michezo inaweza kuwa jukwaa muhimu la kutangaza utalii, kuhamasisha uhifadhi wa maliasili na kuijenga Tanzania kama moja ya maeneo bora ya utalii barani Afrika.
Dkt. Mtae alihitimisha kwa kueleza matarajio ya NCAA kuona ushirikiano huo ukidumu kwa muda mrefu na kuleta manufaa kwa pande zote mbili pamoja na taifa kwa ujumla.
"Karibuni Nyumbani, Karibuni Ngorongoro," alisisitiza.


No comments:
Post a Comment