Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema juhudi za kuimarisha afya na uhai wa wanawake, watoto wachanga na watoto ni muhimu katika kujenga afya bora, nguvu kazi na maendeleo endelevu barani Afrika.
Mhe. Ndejembi amesema hayo tarehe 23 Septemba 2026 jijini New York, Marekani, katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu kwa ajili ya uhai wa mama na mtoto barani Afrika, ulioandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Amesema Afrika bado inakabiliwa na kiwango kikubwa cha vifo vya mama na watoto, licha ya kuwepo kwa hatua za maendeleo katika huduma za afya. Kwa mujibu wa hotuba hiyo, Afrika inachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani na karibu theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano, huku vifo vingi vikiwa vinaweza kuzuilika.
Mhe. Ndejembi amesema Ajenda ya Sifuri Tatu inalenga kufikia sifuri ya kujifungua nyumbani bila msaada wa mtaalamu mwenye ujuzi, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto mchanga, na sifuri ya watoto wasiopata chanjo. Amesema utekelezaji wake unahitaji huduma bora za afya ya msingi, wataalamu wenye ujuzi, mifumo ya rufaa, dawa na vifaa muhimu pamoja na fedha zinazofika katika ngazi ya utoaji huduma.
Aidha, amesema Tanzania imeendelea kupata uzoefu katika kuimarisha huduma za afya ya msingi na dharura za mama na mtoto mchanga, mfumo wa rufaa wa kidijitali wa m-Mama, pamoja na ufuatiliaji wa vifo vya kina mama na watoto. Ameeleza kuwa uzoefu huo unaonesha umuhimu wa kuunganisha uongozi wa kisiasa, uwekezaji na utekelezaji wenye uwajibikaji ili kuboresha matokeo ya afya.
Mhe. Ndejembi ametoa wito wa kuimarisha uwajibikaji wa kisiasa, kuongeza uwekezaji katika huduma zinazookoa maisha na kuhakikisha ahadi zinafikia ngazi ya utekelezaji nchini. Amesema hakuna mwanamke anayepaswa kupoteza maisha kwa kukosa usafiri, damu au huduma yenye ujuzi, wala mtoto anayepaswa kupoteza maisha kwa kukosa huduma inayoweza kuokoa maisha au chanjo, akisisitiza kuwa “Jiongeze Tuwavushe Salama” ni wito wa kuchukua hatua kwa ajili ya kila mama, mtoto mchanga, mtoto na kijana.

.jpeg)

.jpeg)



.jpeg)
No comments:
Post a Comment