Thursday, September 24, 2026

GEITA YAWAKA: TUME YA MADINI YAFUNGUA DIRISHA LA FURSA KWA WAWEKEZAJI NA WANANCHI









Wadau wa madini, wawekezaji na wananchi kwa ujumla wamealikwa kutembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Kitaifa ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili mkoani Geita, kuanzia Septemba 23 hadi Oktoba 3, 2026.

Banda hilo limekuwa sehemu muhimu kwa wananchi wanaotaka kujifunza na kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini, huku likitoa nafasi kwa wachimbaji, wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kuzungumza na wataalamu na kupata ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Tume ya Madini.

Katika maonesho hayo, wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini, shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, uchenjuaji pamoja na biashara ya madini na taratibu mbalimbali zinazohusiana na shughuli hizo.

Moja ya vivutio vinavyowavutia wananchi katika banda hilo ni Maabara ya Tume ya Madini, inayotoa elimu kuhusu huduma za upimaji na uchambuzi wa madini kwa kutumia teknolojia mbalimbali, ikiwemo mashine ya XRF inayotumika katika upimaji wa madini ya metali.

Kwa wananchi wengi, fursa hiyo inawapa nafasi ya kuona kwa vitendo namna teknolojia inavyotumika katika kutambua na kuchambua madini, huku wachimbaji na wafanyabiashara wakipata uelewa kuhusu umuhimu wa kupima madini na kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi ya kibiashara na uwekezaji.

Aidha, wageni wanaotembelea banda la Tume ya Madini wanapata nafasi ya kukutana na wadau wa madini waliofanikiwa, kusikiliza uzoefu wao na kujifunza namna walivyobadilisha fursa za madini kuwa shughuli zenye tija na manufaa kiuchumi.

Ushuhuda huo unaifanya safari ya kutembelea banda hilo kuwa zaidi ya kutazama maonesho, kwani wananchi wanapata nafasi ya kujifunza, kuuliza maswali, kupata ushauri wa kitaalamu na kuona fursa mbalimbali zinazopatikana katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini.

Kwa mwekezaji anayetafuta fursa mpya, mchimbaji anayehitaji elimu na huduma za kitaalamu, mfanyabiashara anayetaka kufahamu taratibu za biashara ya madini au mwananchi anayetamani kuelewa zaidi kuhusu Sekta ya Madini, maonesho hayo yanatoa fursa ya kupata taarifa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa Tume ya Madini.

Tume ya Madini inawahimiza wananchi na wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo kwa kutembelea banda lake katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili, Geita, na kujifunza zaidi kuhusu fursa, teknolojia, huduma na mafanikio katika Sekta ya Madini kabla ya kufungwa kwa maonesho hayo Oktoba 3, 2026.

No comments:

MHE. NDEJEMBI: SIFURI TATU NI MUHIMU KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Sami...