Serikali na Kampuni ya Barrick Corporation zimeendelea kuimarisha ushirikiano wao wa kibiashara na uwekezaji katika sekta ya madini, huku pande hizo mbili zikisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira yatakayowezesha miradi inayotekelezwa kupitia Twiga Minerals Corporation Limited (TWIGA) kukua, kuongeza uzalishaji na kutoa manufaa endelevu kwa Taifa na wawekezaji.
Mwelekeo huo umejitokeza Jumanne, Septemba 1, 2026, wakati Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alipokutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Barrick Corporation pamoja na uongozi wa TWIGA katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalijikita katika maendeleo ya biashara, uendeshaji wa miradi na masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji unaosimamiwa kupitia TWIGA, kampuni inayowakutanisha Serikali na Barrick kama wanahisa wenza katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu nchini.
Miradi iliyojadiliwa ni pamoja na migodi ya North Mara na Bulyanhulu, pamoja na Buzwagi, ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho za kufungwa.
Ujumbe wa Barrick uliongozwa na Roelie Gey Von Pittius, Meneja wa Fedha wa Barrick kwa Afrika na Mashariki ya Kati, akiambatana na Candace Simpson, Meneja wa Kodi wa Afrika na Mashariki ya Kati; Melkiory Ngido, Meneja wa Barrick nchini Tanzania; na Judith Chambua, Meneja wa Kodi wa Barrick Tanzania.
Barrick Gold Corporation ni moja ya kampuni kubwa zaidi duniani za uchimbaji wa madini ya dhahabu na shaba, ikiwa na makao makuu yake mjini Toronto, Ontario, Canada.
SERIKALI YATAKA UBIA WENYE TIJA NA UENDELEVU
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mchechu alisema Serikali, kupitia OTR, itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi ya TWIGA, kwa lengo la kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa kwa ufanisi na kuendelea kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania.
Alisema sekta ya madini ina nafasi muhimu katika ukuaji wa uchumi na mapato ya Serikali, ikiwemo kupitia gawio linalotokana na uwekezaji wa Serikali katika kampuni zinazofanya shughuli za madini.
“Tunauthamini sana mchango wa aina ya ushirikiano tulionao na Barrick,” alisema Bw. Mchechu.
Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, uzoefu uliopatikana kupitia ushirikiano na Barrick umeendelea kuwa muhimu katika kuimarisha uwezo wa Serikali kusimamia uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini na kujenga ubia wenye manufaa kwa pande zote.
Alisisitiza pia umuhimu wa taasisi za Serikali kuwa na uratibu na uelewa wa pamoja katika kushughulikia masuala yanayogusa uwekezaji mkubwa wa kimkakati.
“Katika masuala muhimu kama haya yanayomhusu mshirika muhimu katika biashara muhimu, ni lazima Serikali izungumze kwa sauti moja,” alisema.
UWEKEZAJI WA MUDA MREFU
Bw. Mchechu alisema dhamira ya Serikali ni kuona mazingira ya biashara na uwekezaji yanaendelea kuwa na uthabiti unaowezesha kampuni kufanya mipango ya muda mrefu na kuendeleza uwekezaji wenye manufaa kwa vizazi vijavyo.
“Tunataka kuwa na biashara ambayo inaweza kuendelea kwa utulivu kizazi hadi kizazi na kustahimili tawala mbalimbali za kisiasa,” alisema.
Kauli hiyo inaweka msisitizo katika kujenga uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara, wenye msingi wa mazungumzo, uelewa wa pamoja na mazingira yanayowezesha uwekezaji kuendelea kukua.
Kwa upande wake, Von Pittius alisema Barrick inathamini ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania na itaendelea kufanya kazi kwa karibu na mamlaka husika katika masuala yanayohusu shughuli na uwekezaji wake nchini.
Alieleza utayari wa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali katika maeneo yenye maslahi ya pamoja kwa maendeleo ya sekta ya madini.
Mazungumzo hayo yanaendeleza ushirikiano kati ya Serikali na Barrick katika kuimarisha TWIGA kama jukwaa la ubia wa kibiashara, huku msisitizo ukiwekwa katika kuongeza ufanisi, uzalishaji na thamani inayotokana na rasilimali za madini kwa manufaa ya Taifa na wadau wa uwekezaji.


No comments:
Post a Comment