Monday, September 28, 2026

CP KOMBO AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAAFISA HABARI WA JESHI LA POLISI

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo amewataka Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi kuendelea kuwa nguzo imara katika kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu masuala ya ulinzi na usalama.

Hayo amezungumza Septemba 28, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu kwa Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi wa Makao Makuu ya Polisi, Mikoa, Vikosi na Vyuo vya Polisi katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.

CP Kombo amehimiza nafasi ya Maafisa Habari katika kujenga na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na jamii, huku akiwataka kutumia taaluma yao kuhakikisha umma unapata elimu na taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu Jeshi la Polisi ikiwemo kazi na mafanikio.

"Ninyi ni kiungo muhimu sana kati ya Jeshi la Polisi na jamii, kazi yenu sio tu kutoa taarifa bali kuwajengea uelewa wananchi kuhusu majukumu ya Jeshi la Polisi, changamoto zake, mafanikio yanayopatikana na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao" alisema CP Kombo 

Naye, Kamishna wa Polisi Jamii CP Alex Mkama amesema kuwa kitengo cha habari na uhusiano ndani ya Jeshi la Polisi kimekuwa na mchango mkubwa katika kuzuia na kutanzua uhalifu kwani jamii imekuwa ikihabarishwa na kujengewa uwezo wa kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu kabla haujatokea katika maeneo yao.

CP Mkama aliongeza kuwa, Maafisa Habari wa Mikoa wamekuwa msaada mkubwa sana kufikisha kwa umma elimu ya Polisi Jamii inayotolewa na Maafisa Polisi Jamii wa Mikoa, Wilaya na Polisi Kata na kuahidi kuendelea kushirikiana nao ili kuongeza chachu zaidi na kupata mafanikio zaidi katika kuzuia na kutanzua uhalifu.

Akitoa neno la utangulizi katika hafla ya ufunguzi wa kikao kazi hicho, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime amesema kuwa Afisa Habari wa Jeshi la Polisi amekuwa ni mtu muhimu katika kuandaa na kusambaza maudhui sahihi ya kuelimisha na kutangaza mafanikio na majukumu ya Jeshi la Polisi.

DCP Misime aliongeza kuwa, utendaji kazi wa Maafisa habari wa Polisi umeleta matokeo chanya katika jamii kwani wameendelea kuwa kiungo muhimu kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, wamekuwa chachu katika uandaaji na utoaji wa taarifa kwa wakati, upigaji picha za kihabari na kuandaa maudhui ya uelimishaji jamii na kuainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu nchini.

Kikao kazi cha Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi nchini kimelenga kuwajengea uwezo, uelewa Maafisa habari wa Polisi na kuimarisha mahusiano mazuri kati yao na vyombo vya habari nchini katika kuhabarisha umma kwa kutumia njia za kidigitali na kujenga taswira chanya ya Jeshi la Polisi Tanzania kwa wananchi.







No comments:

CP KOMBO AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAAFISA HABARI WA JESHI LA POLISI

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo amewataka Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi kuendelea kuwa nguzo imara katika kuelimisha n...