Friday, September 25, 2026

DKT. MWIGULU ATEMBELEA VATICAN CITY

 DKT. MWIGULU ATEMBELEA VATICAN CITY






ROMA, ITALIA, Septemba 24, 2026
— Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametembelea Vatican City akiwa jijini Roma, Italia, ambako alikuwa katika ziara ya kikazi iliyohusisha ushiriki wake katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo.

Akiwa Vatican City, Waziri Mkuu alikutana na Mkuu wa Itifaki wa Sekretarieti ya Nchi ya Vatican, Monsinyori Javier Domingo Fernández González, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mji huo.

Ziara hiyo imefanyika baada ya Dkt. Mwigulu kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo uliofanyika Septemba 21–23, 2026 katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma. Katika mkutano huo, Dkt. Mwigulu alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo wa kimataifa uliwakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu, wakulima, vijana, wawakilishi wa asasi za kiraia na wadau wengine kutoka maeneo mbalimbali duniani kujadili namna ya kuimarisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja (One Health) katika mifumo ya chakula na kilimo. Dhana hiyo inatambua uhusiano wa karibu uliopo kati ya afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

Katika ziara yake Vatican City, Waziri Mkuu pia alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali yenye historia na urithi mkubwa wa kiutamaduni na kidini. Vatican City inatambulika duniani kama kitovu cha Kanisa Katoliki na makao ya uongozi wake.

Ziara hiyo imekuwa sehemu ya ratiba ya Dkt. Mwigulu akiwa Roma, ambako pamoja na kushiriki mkutano wa FAO, alifanya mazungumzo na viongozi na wadau mbalimbali wa kimataifa kuhusu masuala ya maendeleo, kilimo, afya na mifumo endelevu ya chakula.

Awali, Dkt. Mwigulu alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu, ambapo pamoja na mambo mengine walijadili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na FAO katika kuendeleza sekta ya kilimo na mifumo ya chakula. Mazungumzo hayo yaligusa maeneo kama kuongeza uzalishaji, mifugo, uvuvi na ufugaji wa viumbe majini, ubora wa mbegu na mbolea, matumizi ya teknolojia na zana za kisasa za kilimo pamoja na kuimarisha uwezo wa wakulima wadogo.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo pia uliweka msisitizo katika umuhimu wa kuunganisha sekta mbalimbali katika kukabiliana na changamoto zinazohusu afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira, sambamba na kuimarisha usalama wa chakula na ustahimilivu wa mifumo ya kilimo.

Dkt. Mwigulu aliwasili Roma Septemba 20, 2026 kwa ajili ya kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo wa kimataifa.

No comments:

JETOUR G700 YAJITOKEZA KWA UWEZO MKUBWA KWA MAZINGIRA YA AFRIKA

  Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam JETOUR Tanzania imezindua rasmi JETOUR Club pamoja na kutambulisha magari mapya ya JETOUR G700 na F700, i...