Friday, June 12, 2026

RAIS SAMIA AIPONGEZA BOT KWA KUKUSANYA DHAHABU YA THAMANI YA TSH TRILIONI 10, ATOA MAELEKEZO MAPYA KUHUSU MIKOPO KWA WANANCHI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba kwenye Maadhimisho ya cha miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya Kitabu cha picha za matoleo ya noti kuanzia mwaka 1966-2026, pamoja na Sarafu ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania kutoka kwa Gavana wa Benki hiyo Bw. Emmanuel Tutuba katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya Kitabu cha picha za matoleo ya noti kuanzia mwaka 1966-2026, pamoja na Sarafu ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania kutoka kwa Gavana wa Benki hiyo Bw. Emmanuel Tutuba katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo Maalum kutoka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba kwenye Maadhimisho ya cha miaka 60 ya Benki hiyo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mafanikio makubwa ya kukusanya tani 27.05 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 10, hatua aliyoitaja kuwa ya kimkakati katika kuimarisha uchumi wa Taifa na kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.

Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Juni 12, 2026, wakati akihutubia kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

"Nipongeze Benki Kuu kwa mpango wa ununuzi wa dhahabu ya ndani. Hadi mwezi Mei mwaka huu tumefanikiwa kukusanya tani 27.05 za dhahabu zenye thamani ya shilingi trilioni 10. Hapa tulipofika si haba," amesema Rais Samia huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha akiba ya Taifa.

Ameeleza kuwa mkakati wa kununua dhahabu kutoka ndani ya nchi umeiwezesha Tanzania kuongeza uwezo wa kukabiliana na misukosuko ya uchumi wa dunia huku ukiimarisha akiba ya fedha za kigeni na kuongeza uthabiti wa mfumo wa kifedha.

Katika hotuba yake, Rais Samia ameitaka Benki Kuu kuendelea kusimamia kwa karibu sekta ya fedha ili kuhakikisha mfumuko wa bei unaendelea kudhibitiwa na uchumi wa nchi unaendelea kukua kwa manufaa ya wananchi wote.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia na ubunifu wa kidijitali katika sekta ya fedha ili huduma za kifedha ziweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi, hususan waliopo maeneo ya vijijini na pembezoni.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa maelekezo muhimu kwa Benki Kuu na taasisi za fedha nchini kutafuta njia mbadala za kuwawezesha wananchi kupata mikopo hata kama hawana dhamana za kawaida kama nyumba, viwanja au magari.

Amesema wananchi wenye biashara zinazoonekana, historia nzuri ya mauzo pamoja na rekodi za miamala wanapaswa kupewa nafasi ya kupata mikopo kwa kuzingatia kiwango chao cha uaminifu na uwezo wa kurejesha fedha.

"Tusimnyime mtu mkopo kwa sababu hana mali tulizozizoea wakati ana historia inayoonesha wazi kuwa anaaminika. Uaminifu ni mali kubwa kuliko hata mali inayoonekana," amesisitiza Rais Samia.

Kauli hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wadau wa uchumi na biashara, ikitarajiwa kufungua fursa zaidi kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ambao mara nyingi hukosa mikopo kutokana na kutokuwa na dhamana za jadi zinazotakiwa na taasisi za fedha.

Maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yamekuwa fursa ya kutafakari mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa huku yakifungua ukurasa mpya wa mageuzi yanayolenga kujenga mfumo wa kifedha unaojumuisha wananchi wengi zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi unaogusa maisha ya kila Mtanzania.

No comments:

CGP. KATUNGU AWATAKA MAAFISA USTAWI KUELIMISHA WAFUNGWA HAKI NA WAJIBU WAO

  Na. Ssgt Mawazo Mtondo – Dodoma. Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii wa Jeshi la Ma...