
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la Tiba Mionzi (Radiotherapy Unit) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro tarehe 24 Juni, 2026. Uzinduzi huu unaashiria hatua kubwa ya kuimarisha huduma za matibabu ya saratani nchini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa katika mikoa ya Kaskazini na Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Gehaz Malasusa, kuashiria uzinduzi wa Jengo la Tiba Mionzi (Radiotherapy Unit) katika Hospitali ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro tarehe 24 Juni, 2026. Uzinduzi huu unaashiria hatua kubwa ya kuimarisha huduma za matibabu ya saratani nchini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa katika mikoa ya Kaskazini na Afrika Mashariki.
Kilimanjaro, 24 Juni 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na taasisi za afya, itaendelea kupanua huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani katika kanda mbalimbali za nchi ili kupunguza mzigo wa safari, gharama za matibabu na msongamano wa wagonjwa katika vituo vya matibabu nchini.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa jengo la tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Ameeleza kuwa kuanza kwa huduma za tiba mionzi katika Hospitali ya KCMC ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kusogeza huduma maalum na za kibingwa za afya karibu na wananchi, ili kuhakikisha matibabu bora yanapatikana kwa wakati na kwa watu wengi zaidi.
“Tulikuwa na kituo kimoja cha tiba ya saratani cha Ocean Road. Huduma hizo sasa zimefikishwa katika Hospitali za Bugando na KCMC; na tunaendelea kuzifikisha katika kanda nyingine ili wananchi wasilazimike kutegemea kituo kimoja pekee,” amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imechangia Shilingi bilioni 5.5 kufanikisha sehemu ya ujenzi na manunuzi ya vifaa vya mradi huo, na itaendelea kushirikiana na KCMC katika kuongeza ufanisi wa huduma hiyo kwa wananchi.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya, kuongeza huduma za uchunguzi wa awali wa saratani, na kutoa wito kwa wananchi kuondoa hofu ya uchunguzi kwa kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara, sambamba na kusisitiza umuhimu wa elimu ya afya kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa saratani.
Rais Dkt. Samia pia amesisitiza umuhimu wa uchunguzi wa awali wa saratani, hususan kwa aina ya saratani za mlango wa kizazi, matiti, tezi dume na koo, ambazo ni miongoni mwa saratani zinazoonekana zaidi nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amepongeza hatua nzuri iliyofikiwa ya ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Magonjwa ya Moyo KCMC, na kuzitaka taasisi za utafiti wa afya nchini kufanya utafiti wa kina kuhusu ongezeko la saratani na magonjwa ya moyo kwa watoto ili kusaidia hatua za kinga, tiba na utoaji wa elimu kwa umma.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuanza kwa huduma za tiba mionzi KCMC tangu mwezi Februari mwaka huu, kumeongeza uwezo wa nchi kutoa matibabu ya saratani nje ya jiji la Dar es Salaam na kusaidia kupunguza utegemezi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Foundation for Cancer Care in Tanzania (FCCT), Bi. Hazel Reinhardt, amesema mradi huo umeiwezesha KCMC kuwa sehemu ya mtandao wa vituo vinavyotoa huduma jumuishi za saratani, hatua inayopanua upatikanaji wa matibabu kwa wananchi wengi zaidi, akiitaja hatua hiyo muhimu kuwa ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, KCMC, FCCT na wafadhili wake.
Naye, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Alex Malasusa, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Hospitali ya KCMC katika kuimarisha miundombinu, vifaa tiba na huduma za afya nchini.
Halikadhalika, ameiomba Serikali kuendelea kuunga mkono hatua zinazofuata za upanuzi wa huduma katika hospitali hiyo, ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya awamu ya pili vya tiba mionzi na utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Kisasa cha Magonjwa ya Moyo unaoendelea kujengwa hospitalini hapo.





No comments:
Post a Comment