Friday, June 05, 2026

Samia Aitangaza Tanzania kama Kitovu cha Uwekezaji Afrika katika Kongamano la Biashara Tanzania na Urusi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika Jijini St. Petersburg nchini Urusi tarehe 05 Juni, 2026. Kongamano hilo limewakutanisha Wafanyabiashara, Wawekezaji pamoja na Taasisi za kukuza Uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi.





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha fursa za biashara na uwekezaji barani Afrika kwa kuwasilisha maono ya nchi katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika jijini St. Petersburg nchini Urusi tarehe 05 Juni, 2026.

Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji na taasisi za kukuza uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi, Rais Samia alieleza mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyapata katika kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha miundombinu ya kimkakati na kufungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania imeendelea kuwa moja ya nchi zenye mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na utulivu wa kisiasa, sera zinazovutia uwekezaji, pamoja na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta za usafirishaji, nishati, makazi, utalii, kilimo na viwanda.

Kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji wenye lengo la kuchochea ushirikiano mpya, kuongeza mtiririko wa mitaji, teknolojia na ujuzi utakaosaidia kukuza uchumi wa pande zote mbili.

Kupitia diplomasia ya uchumi inayoongozwa na Rais Samia, Tanzania inaendelea kujijengea nafasi ya kipekee katika ramani ya uwekezaji duniani, huku ikiwavutia wawekezaji wengi zaidi kuja kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za maendeleo. Ushiriki wa Tanzania katika kongamano hilo unaonesha dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendelea kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa, kuongeza biashara na kuharakisha maendeleo ya uchumi kwa manufaa ya wananchi.

Kongamano hilo linatarajiwa kuibua fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi, na kuimarisha zaidi mahusiano ya muda mrefu yaliyopo kati ya mataifa hayo mawili.

No comments:

KIPANGULA: WAHITIMU WA HABARI WATAFAIDIKA NA MABORESHO YA KANUNI

  Na Mwandishi Wetu Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewashauri Waandishi ...