Na Calvin Katera, Arusha
Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 yameendelea kuthibitisha nafasi yake kama jukwaa muhimu la kukuza utalii wa Tanzania kwa kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi, huku yakichangia kuongezeka kwa watalii, uwekezaji na fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo.
Akifungua rasmi maonesho hayo Juni 5, 2026 katika Viwanja vya Magereza jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Utalii Dkt. Thereza Mugobi alisema kuwa Karibu-KiliFair si maonesho ya kawaida bali ni uwekezaji wa kimkakati unaoendelea kuijenga Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.
Alisema kupitia maonesho hayo, mahusiano ya kibiashara yanayojengwa kati ya wadau wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali yamekuwa chachu ya kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka maeneo ya utalii.
"Karibu-KiliFair ni zaidi ya maonesho; ni uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa utalii wa Tanzania. Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya utalii ikiwemo malazi, viwanja vya ndege na barabara ili kuboresha uzoefu wa watalii na kuwafikisha kwa urahisi katika vivutio mbalimbali vya utalii," alisema Dkt. Mugobi.
Aidha, alibainisha kuwa Wizara itaendelea kutumia majukwaa ya kidijitali kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko mbalimbali duniani ili kuongeza ushindani wa nchi katika soko la utalii la kimataifa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo, alisema maonesho hayo yameendelea kuwa daraja muhimu linalowaunganisha mawakala wa utalii, waongoza watalii na wawekezaji wa ndani na wale kutoka masoko ya kimataifa, hatua inayofungua fursa mpya za biashara na ushirikiano.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TANAPA, Dkt. Beatrice Kessy, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, alisema ushiriki wa TANAPA katika Karibu-KiliFair unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kujifunza mwenendo wa masoko ya utalii na uwekezaji pamoja na kupanua wigo wa fursa zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa.
"Kupitia mikutano na majadiliano ya kibiashara yanayofanyika katika maonesho haya, TANAPA hujenga mahusiano mapya na wadau wa sekta ya utalii duniani, huku ikiendelea kutangaza vivutio vya kipekee vilivyopo katika Hifadhi za Taifa za Tanzania," alisema Dkt. Kessy.
Karibu-KiliFair imeendelea kuwa moja ya majukwaa makubwa ya utalii Afrika Mashariki, ikiiwezesha Tanzania kuonesha utajiri wake wa vivutio vya asili, kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta hiyo na kuvutia watalii pamoja na wawekezaji zaidi kutoka sehemu mbalimbali duniani.




.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment