Naibu Waziri wa Maji, Eng. Kundo Mathew, amepongeza juhudi zinazofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuhifadhi misitu na kulinda vyanzo vya maji nchini, akieleza kuwa uhifadhi wa misitu ni msingi muhimu wa upatikanaji endelevu wa maji kwa wananchi na shughuli za maendeleo.
Eng. Kundo alitoa pongezi hizo Juni 4, 2026, alipotembelea banda la TFS na Idara ya Misitu na Nyuki katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea jijini Dodoma.
Akipokea maelezo kutoka kwa Afisa Uhifadhi Mwandamizi wa TFS, Filipo Mwampamba, Naibu Waziri huyo alitaka kufahamu kwa kina namna TFS inavyoshirikiana na Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zinazohusika na usimamizi wa mabonde ya maji katika kuhifadhi vyanzo vya maji vinavyotegemewa kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, uzalishaji wa umeme na shughuli nyingine za kiuchumi.
Akijibu, Mwampamba alisema TFS imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za kuhifadhi misitu ya vyanzo vya maji kwa kushirikiana na mamlaka za mabonde ya maji, serikali za mitaa na wadau wa maendeleo.
Alisema ushirikiano huo unajumuisha upandaji miti, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa, kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazochangia uharibifu wa mazingira pamoja na utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka hifadhi za misitu.
“Misimu mingi ya mvua na upatikanaji wa maji hutegemea uwepo wa misitu yenye afya. Misitu mingi inayosimamiwa na TFS ndiyo chanzo cha mito na chemchemi zinazolisha mabonde makubwa ya maji nchini,” alisema Mwampamba.
Aliongeza kuwa TFS pia ina jukumu la kusimamia na kuhifadhi hifadhi za misitu, kuendeleza ufugaji nyuki na biashara ya mazao ya nyuki, pamoja na kusimamia utalii ikolojia na maeneo ya urithi wa kihistoria yaliyopo ndani ya hifadhi za misitu.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Eng. Kundo alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa TFS katika kulinda mazingira na kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kuwa salama kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Uhifadhi wa misitu ni sehemu muhimu ya uhifadhi wa rasilimali za maji. Bila misitu imara, upatikanaji wa maji ya uhakika kwa wananchi, viwanda na miradi ya uzalishaji wa umeme unaweza kuathirika. Tunapongeza kazi kubwa inayofanywa na TFS katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kulindwa,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri mifumo ya ikolojia na upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kupunguza uharibifu wa misitu na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali asilia kwa maendeleo ya taifa.




No comments:
Post a Comment