Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk. Sophia Kongela nyenzo za kazi wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Hamad Abdallah anashuhudia.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza na Bodi Mpya wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).Na Mwandishi Wetu, Arusha
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, amezindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuitaka kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Shirika, kuongeza kasi ya ukusanyaji wa madeni pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi ya makazi nafuu ili kukidhi mahitaji ya Watanzania.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Arusha, Dk. Akwilapo alisema NHC ni taasisi muhimu katika utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, salama na yanayomudu gharama za maisha ya wananchi wa kipato cha kati na cha chini.
Waziri huyo alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio makubwa ambayo Shirika limeendelea kuyapata katika uwekezaji na usimamizi wa miradi, bado kuna umuhimu wa kuimarisha nidhamu ya kifedha hususan katika ukusanyaji wa mapato na madeni yanayodaiwa na Shirika.
"Hakuna mdaiwa anayepaswa kuogopwa. Madeni yote halali yanapaswa kufuatiliwa na kulipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa. Uimara wa Shirika unategemea uwezo wake wa kusimamia rasilimali zake na kukusanya mapato yake kwa wakati," alisema Dk. Akwilapo.
Aliwaagiza NHC kutoogopa kudai malipo yao ambayo ni halali kwa shirika. "Msimuogope yeyote, hata akawa na cheo gani daini fedha za serikali na mimi nipo tayari kuwasaidia ili Shirika liendelee kutoa huduma bora."
Alibainisha kuwa Serikali ina matarajio makubwa kwa Bodi hiyo mpya katika kusimamia maandalizi na utekelezaji wa Mpango Mkakati mpya wa Shirika, ambao unapaswa kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo pamoja na ajenda ya makazi endelevu duniani.
Dk. Akwilapo pia aliitaka Bodi kuendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa za ujenzi, kuimarisha ubunifu katika upatikanaji wa mitaji ya miradi na kusimamia uwekezaji wa Shirika kwa tija zaidi ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ya NHC inaongozwa na Dk. Sophia Kongela kama Mwenyekiti, huku wajumbe wake wakiwa ni Eliud Sanga, Profesa Wilbard Kombe, Dk. Ali Hussein Laay, Doroth Mwanyika, Ayoub Omari Kasuwi, Vupe Ligate na Elias Kisamo.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi hiyo, Dk. Sophia Kongela alisema wajumbe wamepokea kwa heshima na uzito mkubwa dhamana waliyopewa na Serikali ya kuiongoza NHC katika kipindi hiki muhimu cha maendeleo ya sekta ya makazi nchini.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa jukumu la kusimamia taasisi hiyo, akiahidi kuwa Bodi itafanya kazi kwa weledi, uwazi na uwajibikaji ili kuhakikisha NHC inafikia malengo yake.
"Tutatoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali na Menejimenti ya Shirika ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi, mapato yanaongezeka na NHC inaendelea kuwa taasisi ya mfano katika sekta ya makazi," alisema Dk. Kongela.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alisema Shirika limeendelea kuimarisha nafasi yake kama taasisi ya kimkakati katika maendeleo ya makazi kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya makazi, biashara na uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa NHC imeendelea kuongeza thamani ya mali zake, kuimarisha mifumo ya kidijitali na kusimamia kwa ufanisi rasilimali zake za ardhi, nyumba na majengo ya biashara, hatua ambazo zimechangia kuongezeka kwa mapato na kuimarika kwa utendaji wa Shirika.
Hamad alisema Menejimenti iko tayari kushirikiana na Bodi mpya katika kutekeleza maelekezo ya Serikali na kuhakikisha NHC inaendelea kuwa chombo muhimu katika kutatua changamoto ya makazi nchini.
Katika hotuba yake, Dk. Akwilapo aliipongeza NHC kwa kuendelea kufanya vizuri kibiashara na kiutendaji katika kipindi ambacho baadhi ya mashirika mengi ya umma yaliyowahi kuwa nguzo za uchumi wa Taifa yalishindwa kuhimili ushindani na kutoweka.
Alisema mafanikio ya NHC yanaonesha kuwa taasisi za umma zinaweza kufanya vizuri ikiwa zitasimamiwa kwa nidhamu, uwajibikaji na maamuzi sahihi ya kiutawala na kibiashara.
Uzinduzi wa Bodi hiyo mpya unafungua ukurasa mpya wa utekelezaji wa majukumu ya Shirika la Nyumba la Taifa, huku matarajio makubwa yakiwekwa katika kuongeza upatikanaji wa makazi bora, kuimarisha uwekezaji wa kimkakati na kuchangia maendeleo endelevu ya miji na uchumi wa Tanzania.





No comments:
Post a Comment