Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Cuthbert Sendiga, jana Februari 18, 2025, amezindua rasmi mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika kwa maafisa ushirika wa Kanda ya Kaskazini. Mafunzo haya yatadumu kwa siku 11, huku kwa Mkoa wa Manyara yakitarajiwa kufanyika kwa siku 6.
Mafunzo haya yanawahusisha maafisa kutoka mikoa sita, ambayo ni Manyara, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, na Dodoma. Lengo kuu ni kuwajengea uwezo maafisa hao katika usimamizi wa vyama vya ushirika, uwekezaji, matumizi ya mifumo ya kisasa ya TEHAMA, pamoja na kuimarisha maendeleo ya benki za ushirika.
Aidha, mafunzo haya yanajikita katika kuhimiza uadilifu, maadili ya kazi, utunzaji wa siri za taasisi, na namna bora ya kutatua changamoto zinazoyakabili vyama vya ushirika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Mheshimiwa Sendiga ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuandaa mafunzo haya muhimu. Ameeleza kuwa kupitia mafunzo haya, maafisa ushirika wataongeza ujuzi wao, kujenga uadilifu, na kufanya kazi kwa kujiamini zaidi, hivyo kuchochea maendeleo katika sekta ya ushirika.
Pia, RC Sendiga ameitoa agizo kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha inatatua migogoro inayokwamisha maendeleo ndani ya vyama vya ushirika. Ameeleza kuwa migogoro hiyo inasababisha kudumaa kwa vyama vya ushirika na kuchelewesha maendeleo ya wanachama wake.
Kwa kuhitimisha, Mheshimiwa Sendiga amesisitiza kuwa usimamizi bora wa vyama vya ushirika unapaswa kuzingatia uwajibikaji, matumizi ya teknolojia za kisasa, na uadilifu ili kuvifanya kuwa nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment