Sunday, February 16, 2025

AU Rais Samia Ahimiza Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Kwenye Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi wa




Addis Ababa, Ethiopia – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama njia endelevu ya kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi wa Afrika.

Akizungumza tarehe 16 Februari 2025 katika Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika katika ukumbi wa Nelson Mandela, Makao Makuu ya Umoja huo, Addis Ababa, Ethiopia, Rais Samia alieleza jitihada za Tanzania katika kusambaza nishati safi kwa wananchi wake na akatoa wito kwa mataifa ya Afrika kushirikiana katika kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo.

Katika hotuba yake, Rais Samia alieleza kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa bara la Afrika bado wanategemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia, jambo linalochangia ukataji miti kwa wingi na kuathiri mazingira. 

Alisema kuwa matumizi ya nishati chafu yana madhara makubwa kwa afya, hususan kwa wanawake na watoto ambao mara nyingi wanakabiliwa na moshi unaotokana na kuni na mkaa.

"Tunapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wetu wanapata nishati safi na salama ya kupikia ili kulinda afya zao na mazingira yetu. Tanzania tayari imeanza kutekeleza mikakati madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya gesi ya kupikia, biogas, na vyanzo vingine vya nishati safi," alisema Rais Samia.

Rais Samia pia alibainisha kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza katika miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia nishati hiyo kwa gharama nafuu. 

Alisema kuwa kupitia mipango mbalimbali, ikiwemo ruzuku kwa kaya za kipato cha chini, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati mbadala kwa wananchi wake.

Katika hotuba yake, Rais Samia aliwataka viongozi wa Afrika kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, na taasisi za kifedha ili kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo. 

Alisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, Afrika inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya wananchi wake.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika wa mwaka huu umejikita katika kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo barani Afrika, ikiwa ni pamoja na nishati, uchumi, usalama, na ushirikiano wa kikanda. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha mawaziri na maafisa waandamizi kutoka sekta mbalimbali, wakiwa na dhamira ya kuendeleza maslahi ya taifa na bara kwa ujumla.

No comments:

MHANDISI MRAMBA: BIASHARA YA KUUZIANA UMEME KUINUFAISHA TANZANIA

  📌Afafanua kuuuza na kununua umeme ni jambo la kawaida kwa nchi 📌Asisitiza kununua umeme kwa Mikoa ya Kaskazini kunamanufaa kwa Mikoa hus...