Sunday, February 09, 2025

KAMATI YA PIC YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TAWA ENEO LA MAKUYUNI



















📍 Yathibitisha uwepo wa tija ya uwekezaji

Na Beatus Maganja - Arusha

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Augustine Vuma Holle (Mb) amesema Kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya utalii inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA katika Hifadhi ya eneo la Makuyuni Wildlife Park iliyopo wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.

Mhe. Augustine ameyasema hayo leo Februari 9, 2025 wakati Kamati yake ilipotembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAWA  katika eneo hilo.

"Kamati imefurahishwa na namna ambavyo miradi inaendelea, ikumbukwe kwamba hili eneo mara ya kwanza lilikuwa chini ya mwekezaji Kwa muda mrefu sana, baada ya Serikali kuona kwamba hakuna tija eneo hili kuendelea kukaa Kwa mwekezaji, ikalichukua eneo hili na kukabidhiwa msajili wa hazina lakini baadae msajili wa hazina aliwakabidhi TAWA ili waweze kuliendeleza" amesema Mhe. Augustine 

"Kamati imeona na imeshuhudia pasipo na shaka kwamba uwekezaji unafanyika na unafanyika kwa utaratibu ambao unafaa na kwakweli tija ya uwekezaji ipo kwasababu mapato yameanza kuongezeka na tunaamini yataendelea kuongezeka. Kwahiyo TAWA wataendelea kufanya uwekezaji hapa kwasababu tumeona kwamba imeanza kulipa" ameongeza

Aidha Mwenyekiti huyo wa Kamati ya PIC ametoa wito Kwa watanzania wote na wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani na Arusha kutembelea eneo hilo ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.

"Nitoe rai kwa watanzania wote, kwakweli Makuyuni Wildlife Park ni sehemu nzuri sana ya kuja kutembelea, yaani ukija humu ndani hutamani kutoka, kuna wanyamapori wa kila aina kuna twiga, tumeona simba, tembo, swala kwakweli ni kituo cha kuvutia watalii" amesema

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula  amesema tangu TAWA ikabidhiwe eneo hilo Idadi ya wanyamapori imeongezeka Kwa kiasi kikubwa  na pia fedha zinazotokana na uwekezaji uliofanyika zimeongezeka ambapo amesema kuwa Kwa kipindi cha Mwaka mmoja TAWA imeweza kukusanya zaidi ya shillingi Millioni 200 jambo ambalo linathibitisha kuwa ni mwanzo mzuri na wenye kuleta matumaini makubwa.

Sambamba na hilo Mhe. Kitandula amesema kutokana na uwekezaji unaondelea kufanywa na TAWA Wizara inatarajia TAWA kuongeza mapato ya zaidi ya Billioni 20 Kwa mwaka jambo ambalo Taasisi hiyo imeihakikishia Wizara kuwa inawezakana.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis R. Semfuko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuipatia TAWA eneo la Makuyuni Wildlife Park ili iweze kulitumia Kwa ajili ya shughuli za utalii.

Vilevile Semfuko amesema TAWA imejijengea utamaduni wa kuwa na matumizi sahihi ya fedha hasa fedha zinazotolewa na Serikali Kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

"Hii ndio tabia yetu TAWA kuhakikisha ya kwamba kila senti ambayo Mheshimiwa Rais anaitoa inatumika kama ilivyopangwa na Kwa ubunifu mkubwa" amesisitiza Semfuko

No comments:

RAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AMTEMBELEA MWALIMU ALIYANI

    RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalumu ya msahafu na Mwanazuoni ...