Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Wakala
wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula nchini (NFRA) unatarajia kuuza
takribani tani milioni moja za chakula kwa mwaka wa fedha wa 2025/ 2026
kupitia masoko yaliyopo kwenye nchi tofauti zenye mikataba ya kuuziana
mazao na shirika hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki,
Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dkt Andrew Komba amesema kuwa moja ya majukumu
ya shirika hilo ni kuhakikisha usalama wa kutosha wa chakula hapa
nchini na kuuza chakula cha ziada kwa nchi zenye uhitaji kama moja ya
sehemu ya kuwawezesha wakulima kiuchumi na nchi kujipatia fedha za
kigeni.
Amesema
kuwa katika kipindi cha miaka minne, NFRA imeweza kuuza takribani tani
600,00 za mahindi , mtama mpunga, dengu na mbaazi kwenye masoko ya
India pamoja na China.
Amesema
mafanikio haya na mipango iliyopo yanatokana na uwezeshwaji uliofanywa
na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu
Hassan katika kulijengea uwezo shirika hilo.
“Miaka minne iliyopita, NFRA ilikuwa na uwezo wa kuuza kati ya tani 50,000-60,000 tu za nafaka,”
“Lakini
baada ya kujengewa uwezo, ufanisi uliongezeka ambapo miaka miwili
iliyopita tuliweza kuuza tani 600,000 baada ya wananchi kuanza kufanya
kilimo chenye tija na kuzalisha mazao yenye ubora kulingana na
maelekezo ya wataalamu hususani katika kilimo cha Mahindi na Mchele ,” amesema.
Amesema
kuwa jitihadi za NFRA katika kutafuta masoko ya nafaka mwaka 2024
ilifanikiwa kupata mkataba wa kuuza tani 650,000 kwenda Zambia na mpaka
sasa nusu ya tani hizo tayari zimeshapelekwa katika nchi hiyo na
mkataba huu unatarajiwa kufikia ukomo ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Pia
NFRA ilifanikiwa kuuza tani nyingine 500,000 katika soko la Jamhuri ya
Congo (DRC) na kuuza tani nyingine 35,000 kwenye Shirika la Program ya
Chakula duniani (WFP) ambapo kupitia mikataba hii, NFRA kwa ujumla
imefanikiwa kuuza jumla ya tani 1,185,000 kutoka katika mashirika hayo.
Mbali
na masoko yaliyopo katika nchi za Zambia na Congo (DRC), Malawi na
Zimbabwe, Dkt Komba pia amesema kuwa nchi ya Msumbiji pia wametuma
maombi yao ya kutaka kununua mazao katika shirika hilo.
Ameongeza
kuwa tayari nchi ya Malawi imeingia mkataba na NFRA wa kuuziwa
takribani tani 50,000 za chakula na kati ya tani hizo, wameshasaini
makubaliano ya kuchukua tani 20,000 za kuanzia.
“Haya
yote yanafanyika ni juhudi na jitihada za Serikali ya Rais Samia
ambapo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, NFRA imefanikiwa
kupanua ukubwa wa masoko yake katika nchi za kimataifa na kupelekea
kuongeza tija na thamani ya mazao na kilimo chetu nchini” Alisema Dkt Komba na kuongeza;
“Tumekuwa
tukiongeza nguvu ya mauzo yaliyotokana na chakula cha ziada ili kukidhi
uhitaji wa soko la kimataifa ili kuwafaidisha wakulima wengi kutokana
na chakula tunachoki nunua kutoka kwao kwa ajili ya akiba ya chakula
hapa nchini na ziada kuuza nje ya nchi,” amesema.
“
Ni jukumu kubwa la NFRA kutafuta masoko ya nje ya nchi kwa chakula cha
ziada kinachozalishwa hapa nchini, ili kuongeza tija katika kilimo kwa
wazalishaji wote katika mnyorororo wa thamani,” amesema.
Katika
kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo hapa nchini na kuzalisha
chakula cha ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, Dkt Komba amesema
mamlaka hiyo imekuwa ikiwahimiza wananchi kufanya kilimo cha kisasa na
chenye tija ili kuhakikisha mazao yanakuwa yenye ubora unaohitajika
katika masoko ya kimataifa kwani ndio njia pekee itakayo iwezesha NFRA
kupata masoko ya uhakika.
No comments:
Post a Comment