Zanzibar na Arusha Kukuza Utalii Kimataifa Kupitia Tamasha la Kwanza la Utalii na Uwekezaji Zanzibar
Katika jitihada za kukuza soko la utalii kimataifa na kutanua wigo wa utalii nchini Tanzania, Zanzibar na Mkoa wa Arusha wameungana katika kukuza sekta ya utalii kupitia Tamasha la Kwanza la Utalii na Uwekezaji Zanzibar, linalotarajiwa kufanyika tarehe 25 hadi 26 Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Bw. Aris Abbas Manji, amesema kuwa ziara yao mkoani Arusha inalenga kutangaza Tamasha hilo kwa wadau mbalimbali wa utalii ili kuhamasisha ushiriki wao. Bw. Manji alieleza kuwa sekta ya utalii imekuwa moja ya nguzo kuu za uchumi wa Zanzibar, ikichangia asilimia 30 ya pato la taifa.
Amebainisha kuwa kupitia Tamasha hilo, Zanzibar inapanua wigo wa bidhaa za utalii ili kuvutia watalii zaidi na kuchochea uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Aidha, Bw. Manji alisisitiza kuwa Tamasha hili linatoa fursa ya kipekee kwa wadau wa utalii na uwekezaji, sio tu kutoka Zanzibar bali pia kutoka sehemu nyingine za Tanzania, kuja kujifunza, kushirikiana, na kutafuta fursa mpya za kibiashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Paul Makonda, amepongeza ujio wa Tamasha hilo na kueleza kuwa Mkoa wa Arusha upo tayari kushirikiana kwa karibu na Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya utalii inakua zaidi. Mh. Makonda alisema kuwa Arusha, kama kitovu cha utalii nchini Tanzania kutokana na hifadhi zake za wanyamapori na Mlima Kilimanjaro, ina nia ya dhati ya kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji na kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Arusha unalenga kuongeza idadi ya watalii, kutengeneza ajira kwa vijana, na kuinua uchumi wa maeneo hayo mawili.
Vilevile, Mh. Makonda aliwataka wadau wa utalii wa mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi katika Tamasha hilo ili kupata fursa za kipekee za kushirikiana na wenzao kutoka Zanzibar na sehemu nyingine duniani.
Tamasha la Utalii na Uwekezaji Zanzibar linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo, teknolojia, na fursa za kiuwekezaji katika sekta ya utalii, ikiwemo utalii wa urithi, utalii wa michezo, na utalii wa afya. Ni hatua muhimu katika kufungua milango mipya ya soko la utalii kimataifa, na hivyo kulinufaisha taifa zima kwa ujumla.
Comments