Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (Katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) lililopo Wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wakati wa hafla fupi iliyofanyika jijini Mwanza jana. Wengine ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kulia) Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum (wa tatu kulia) Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bi Amina Nassoro Makilagi (wan ne kulia), Mke wa Rais Dkt Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi (kulia kwa Rais Mwinyi) Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ (wa tatu kushoto) pamoja na viongozi wengine wa serikali na benki hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kulia) akipokea zawadi maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Bw Arafat Haji (wanne kushoto) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo lililopo Wilayani Nyamagana mkoani Mwanza iliyofanyika jijini humo jana. Wengine ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa tatu kushoto) Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum (wa pili kulia) Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bi Amina Nassoro Makilagi (wa pili kushoto) Mke wa Rais Dkt Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi (kuliai) pamoja na viongozi wengine wa serikali na benki hiyo.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Kulia) akizungumza kwenye hafla hiyo.
Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum (Kulia) akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwanza: Oktoba 14, 2024: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezindua tawi jipya la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Mwanza huku akibainisha kuwa uwepo wa benki hiyo mkoani humo utaongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi hususani kwa kupanua wigo wa biashara zao kupitia mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Hafla ya uzinduzi wa tawi hilo lililopo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,ilifanyika jana jijini Mwanza ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakiwemo Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Ikulu, Zanzibar, Ally Suleiman Ameir.
Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Mwanaasha Khamis Juma na mwenyeji wao Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bi Amina Nassoro Makilagi aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo. Kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PBZ, Bw Joseph Abdalla Meza aliwaongoza wafanyakazi wa benki hiyo akiwemo Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw Arafat Haji pamoja na wananchi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Dkt Mwinyi aliwahimiza wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kuitumia vema benki hiyo huku akibainisha kuwa muendelezo wa jitihada za benki ya PBZ kujitanua katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara ni sehemu ya mkakati wake wa kutekeleza kwa vitendo dhamira ya serikali ya kuwaunganisha wananchi wa pande zote mbili kiuchumi.
“Uwepo wa benki ya PBZ katika mikoa mbalimbali hapa Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar unaifanya benki hii kuwa daraja muhimu la kuunganisha Muungano kwa vitendo kwa manufaa ya kiuchumi zaidi. Naamini uwepo wa benki hii hapa mkoani Mwanza utafungua fursa za kiuchumi kwa makundi yote wakiwemo wakulima, wafugaji, wajasiriamali, wafanyabiashara, na wafanyakazi wote wa umma na binafsi. Zaidi natarajia kwamba muingiliano wa kibiashara baina ya Zanzibar na mikoa ya kanda ya Ziwa utachochewa zaidi na uwepo wa tawi hili,’’ alibainisha.
Pamoja na kupongeza ufanisi na weledi wa benki hiyo katika utoaji wa huduma zake, Dkt Mwinyi alionyesha kuguswa na uwajibikaji wake kwa kujamii ikiwemo udhamini wa benki hiyo katika sekta ya michezo ikiwemo mpira wa miguu na riadha pamoja na utoaji wa misaada katika sekta za elimu na afya.
“Ni matumaini yangu pia wakazi wa Mwanza watanufaika na uwajibikaji huu kwa jamii unaonyeshwa na benki ya PBZ ,’’ aliongeza.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ Bw Arafat Haji alisema uwepo wa tawi hilo mkoani Mwanza utawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa mkoa huo kupitia unafuu na ubora wa huduma za benki hiyo sambamba na fursa mbali mbali za uwezeshwaji na mikopo kwa makundi yote wakiwemo wakulima, wafugaji, wajasiriamali, wafanyabiashara, na wafanyakazi wote wa umma na binafsi.
“Haikuwa kwa bahati kufungua tawi letu ndani ya mwezi huu na wiki hii, kwani ni mwezi wa kusheherekea huduma kwa wateja na ufunguzi wa tawi letu hili utasaidia kuwasogezea huduma zetu wateja mbali mbali waliopo Mkoa wa Mwanza na mikoa yote ya karibu. Kwa ufunguzi wa tawi letu hili, tunatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya wiki ya utoaji wa huduma kwa wateja inayokwenda na kauli mbiu ya ‘Above and Beyond’ ‘’ alisema.
Bw Arafat alipongeza jitihada za dhati kwa Rais Dkt Mwinyi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kubuni miongozo na Sera nzuri zinazosaidia kuboresha ukuaji wa uchumi nchini na hivyo kuchochea mafanikio ya taasisi za kifedha.
Ikiwa ni benki ya saba kwa ukubwa kwa rasilimali zaidi ya shilingi trilioni 2.3, benki ya PBZ kwa sasa inaendelea kutanua mtandao wake wa matawi ambapo mwaka huu pekee imeweza kufikia mikoa mitatu mipya ikiwemo Morogoro, Mbeya na Mwanza.
“Katika mpango kazi wetu pia tumejipanga kufungua matawi mengine katika mikoa ya Arusha, Tanga na mengineyo.’’ Aliongeza Arafat huku akibainisha kuwa mpaka sasa, huduma za benki hiyo zinapatikana maeneo yote kupitia kadi za VISA, Kadi za Umoja Switch, mawakala waliopo maeneo mbali mbali nchini, kupitia Simu za Mkononi na kupitia mtandaoni yaani ‘Internet Banking’.
Comments