Friday, February 23, 2018

WAZIRI JAFO AAGIZA DARAJA LA CHIPANGA LIKAMILIKE KABLA YA MWEZI JULAI, MWAKA HUU



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Selemani Jafo akiwa na Mbunge wa jimbo la Bahi Omary Badwel na viongozi wengine wa wilaya ya Bahi.
  Daraja la Chipanga linaloendelea kujengwa
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Chipanga.


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Selemani Jafo amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Medes Company Limited na Millenium Master Builders (T) Limited anayejenga daraja la Chipanga wilayani Bahi, kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ifikapo mwezi Julai, mwaka huu bila visingizio vyovyote.

Akikagua ujenzi wa daraja hilo, Jafo amesema awali kazi ya ujenzi wa Daraja hilo ilitarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu lakini kutokana na Mvua zilizokuwa zikinyesha amewaelekeza kukamilisha ifikapo Julai mwaka huu.

Jafo amewaagiza wakala wa barabara vijijini na mijini (TARURA) kukaa na mkandarasi kukubaliana tarehe ya mwisho ya kukamilika kazi hiyo lakini kinachotakiwa ifikapo Julai mwaka huu daraja hilo liwe limekamilika.

Amebainisha kuwa daraja hilo ni kiunganishi cha kata ya Chipanga na Makao makuu ya wilaya ya Bahi na ujenzi wake unagharimu kiasi cha Sh. bilioni 2.11.

Akizungumza katika mkutano wa hadharana wananchi wa Chipanga, Waziri Jafo amewataka wananchi hao kuacha tabia ya kupitisha ng'ombe na majembe ya ng’ombe kwenye barabarani zinazojengwa kwa kuwa wanasababisha uharibifu wa barabara.

Amesema serikali haiwezi kuvumilia uharibifu wowote wa miundombinu ambayo inagharimu gharama kubwa.

No comments: