HESLB YAWAKUMBUSHA WAAJIRI KUZINGATIA SHERIA


 Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB Bw. Phidelis Joseph akizungumza na waandishi habari kuhusiana ufatilialiaji mkopo kwa walionufaika leo jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Bw. Nzinyangwa Mchany (kulia) na Meneja Mawasiliano wa EWURA Bw. Titus Kaguo(katikati) wakionesha ngao ya utambuzi ya utambuzi walioyokabidhiwa leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (kushoto) kutambua mchango wa taasisi katika urejeshaji mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wafanyakazi wanufaika EWURA. 
  Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (kushoto) akimkabidhi Mwakilishi wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Academic, Mariam Mtelesia ngao ya utambuzi wa ushirikiano wao katika kufanikisha kazi ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika ambao ni wafanyakazi katika taasisi yao.
Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB Bw. Phidelis Joseph akiongea leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwakabidhi waajiri ngao za utambuzi wa ushirikiano wao katika kufanikisha kazi ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika wafanyakazi.


Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imewakumbusha waajiri nchini kote kuzingatia matakwa ya Sheria ya bodi hiyo inayowataka kuwasilisha orodha ya majina ya waajiriwa ambao ni wahitimu wa shahada au stashahada ili kuiwezesha Bodi kubaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Akizungumza na waandishi habari wakati wa wa hafla fupi ya kuwatambua baadhi ya waajiri wanaotimiza masharti ya Sheria ya HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo,Abdul-Razaq Badru amesema kuwa sheria hiyo inawataka waajiri kukata asilimia 15 ya mshahara ghafi wa mwajiriwa na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB ndani ya siku 15 baada ya tarehe ya mwisho ya mwezi.

Amesema kuwatunuku ngao ni kutambua mchango wao katika kurejesha mikopo ili kuwasomesha watu wengine na kuwataka waajiri watekeleze sheria hiyo na kuongeza ufanisi wa shughuli za HESLB hususan katika urejeshwaji wa mikopo.

Taasisi zilizokabidhiwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PSPF), Benki ya NMB, Benki ya CRDB, Benki ya Stanbic, Deloitte Tanzania, Kampuni ya Sigara Tanzania, na Kamouni ya Coca Cola Kwanza. Kampuni nyingine ni Vodacom Tanzania, Nokia Solution Tanzania, Shule za Academic, Shule za Al-Hikma na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

“Nyie ni wadau wetu muhimu sana. Tunavyosema tumeongeza makusanyo ya mikopo iliyoiva kutoka wastani wa TZS 2 bilioni kwa mwezi miaka mitatu iliyopita hadi wastani wa TZS 13 hivi sasa ni kwa sababu ya waajiri kama ninyi … tunawashukuru sana,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB katika hafla hiyo.

Amesema takwimu zinaonyesha, Benki za CRDB na NMB kwa pamoja ziliwasilisha kiasi cha TZS 274.4 milioni kama makato ya mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wafanyakazi wao kwa mwezi Disemba, 2017 pekee. Fedha hizi zinaweza kukopeshwa kwa wanafunzi 78 wa elimu ya juu kwa wastani wa TZS 3.5 milioni kwa mwaka ambazo hutolewa na HESLB hivi sasa.   

Aidha amesema baadhi ya waajiri waliokabidhiwa ngao wameanzisha utaratibu nafuu ndani ya mashirika yao unaowawezesha waajiriwa wanaodaiwa mikopo ya elimu ya juu kuchukua hati ya deni HESLB na kulipa kwa mkupuo kwa uwezeshaji wa mwajiri.
Nae Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB Bw. Phidelis Joseph amesema wataendelea kuwatembelea waajiri ili kubadilishana mawazo kwa lengo la kuongeza ufanisi na makusanyo.

“Ni wajibu wetu kuwafikia waajiri popote walipo ili kuwasikia na kubadilishana mawazo ili hatimaye tuwe na waajiri wengi zaidi wanaotimiza matakwa ya kisheria,” aliongeza.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ngao, Mwakilishi wa Nokia Solution Tanzania Bi. Doroth Namuhisa mara baada ya kuajiri, huchukua majina kamili ya mwajiriwa, jina la chuo alichosoma na namba kamili ya mtihani yenye mwaka aliofanya mtihani huo wa kidato cha nne na kuwasilisha HESLB ili wanufaika waweze kubainika.

“Tumejiwekea utaratibu wa kuwasilisha taarifa zote muhimu kwa Bodi ya Mikopo na ndiyo sababu hatupati changamoto kubwa,” alisema Bi. Namuhisa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya Stanbic Bi. Eutropia Vegula ameipongeza HESLB kwa ushirikiano inaowapatia na kuongeza kuwa benki yake imeingiza matakwa ya Sheria ya HESLB katika sera yao ajira kwa kuhakikisha kila mwombaji kazi anafahamika kama ni mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu au hapana. 

Comments