SERIKALI ya Tanzania inalipongeza
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa jitihada na hatua mbalimbali
zinazochukuliwa na shirikisho hilo katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa jana
(Alhamisi, Februari 22, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika
kikao chake na Rais wa FIFA Bw. Gianni Infantino kilichofanyika jijini
Dae es Salaam.
“Serikali tunaunga mkono
mapambano dhidi ya rushwa kwenye michezo pamoja na matumizi mabaya ya
fedha na ya madaraka yanayofanywa na FIFA”.
Waziri Mkuu amesema wanaunga mkono
mapambano hayo ili Taifa liweze kupata mafanikio makubwa katika mpira
wa miguu ikiwa ni pamoja na kupata viongozi wenye maono ya mbali katika
kuendeleza mchezo huo.
Amesema FIFA ambayo ni kitovu cha
mapambano dhidi ya rushwa kwenye michezo , hivyo Tanzania inaiunga mkono
kwa kuhakikisha sekta ya michezo inatumia vizuri fedha zilizopo kwa
ajili ya kuendeleza michezo.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itahakikisha inasimamia matumizi sahihi ya madaraka katika sekta ya
michezo nchini ili kuleta maendeleo kwenye mpira wa miguu.
Serikali inaipongeza FIFA kwa
jitihada za dhati za kuendeleza mpira wa miguu duniani kwa kuwa mipango
mbalimbali ya kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana wadogo wa kike na wa
kiume nchini.
“Tunatambua msukumo wa FIFA wa
kuendelea mpira wa miguu duniani ikiwa ni pamoja na kuboresha viwanja
vya michezo pamoja na maendeleo yote wanayoyafanya katika sekta hiyo.
Pia ameishukuru FIFA kwa kuipa
Tanzania heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17 yatakayofanyika mwakani jijini Dar es Salaam na kwamba
Serikali itayasimamia vizuri na inajiandaa kwa kushinda.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amemshukuru Rais wa FIFA Bw. Infantino kwa niaba ya Rais Dkt John
Magufuli kwa kuendesha mkutano mkubwa wa viongozi wa mpira wa miguu
duniani Tanzania. Mkutano huo ulihusisha Marais na Makatibu Wakuu wa
nchi 21.
Pia alimpongeza Rais wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Bw. Ahmad Ahmad kwa jitihada zake za
anazozifanya katika kuendeleza mpira barani Afrika na kwamba Serikali
ya Tanzania inamuunga mkono.
Rais wa FIFA Bw. Infantino ambaye
ameahidi kuisaidia Tanzania kwa kuboresha miundombinu ya viwanja vya
michezo aliwasili nchini leo alfajiri akiongozana na Rais wa Shirikisho
la Soka Afrika Bw. Ahmad Ahmad kwa ajili ya mkutano wa FIFA uliofanyika
nchini Tanzania February 22, 2018.
Bw. Infantino amewasili kwa mara
ya kwanza Tanzania toka awe Rais wa FIFA na alipokelewa na viongozi
mbalimbali akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dtk.
Harrison Mwakyembe na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa
Bw. Leodger Tenga na Rais wa TFF Bw. Wallace Karia.
Comments