RC Rukwa awaasa watumishi kutotumia vyeo kuwanyanyasa wananchi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo akifafanua namna mtumishi anavyotakiwa kuwajibika pindi anapowahudumia wananchi  (aliyekaa) kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa David Kilonzo. 
 Viongozi wa mashirika ya ya umma na mamlaka mbalimbali za seikali Mkoani Rukwa Waliohudhuria kwenye kikao hicho kilichowakutanisha wakuu wa mamlaka na mashirika ya umma. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amewaasa watumishi wa mashirika ya umma na wakala wa serikali mkoani Rukwa kutotumia vyeo vyao kuwanyanyasa wananchi wanaowahudumia na badala yake wawasaidie kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa bila ya kujali, rangi kabila, dini na hali zao kiuchumi.

Amesema kuwa watumishi wa serikali ni watumishi wa wananchi hivyo wanapaswa kujituma bila ya kujali vyeo vyao kwani vyeo hivyo havitakuwa na maana ikiwa wananchi hawapati huduma wanayoitarajia kutoka katika serikali waliyoiweka madarakani.

“Sisi viongozi wa Serikali lazima tufanye kazi kwa kujituma na kujitoa na tukumbuke kuwa sisi ni watumishi tu, sio watu wa kujivuna ama wabinafsi na kujinadi kwa vyeo vyetu kwamba mimi meneja, daktari sijui nani, vyeo vyetu vitakuwa na maana pale tu tunapokwenda kwa wananchi na kuwapa huduma” Alieleza.

Na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano ipo kuhakikisha kuwa kila kiongozi anayehudumia wananchi anakuwa mtumishi wa wananchi na kuhakikisha kuwa haki inatendeka na kuonya vikali watumishi wanaowahudumia wananchi kwa kutumia lugha chafu.   

Ameyasema hayo kwenye kikao cha muda mfupi kilichowajumuisha viongozi kutoka katika mashirika ya umma, wakala na mamlaka mbalimbali za serikali zilizomo Mkoani humo ili kufahamu matatizo wanayokumbana nayo pindi wanapotimiza wajibu wao wa kuwahudumia wananchi.

Sambamba na hayo Mh. Wangabo amewataka watumishi wote Mkoani humo kuzingatia muda na kutekeleza kwa wakati mipango waliyojiwekea ili kazi zizae matunda na kutoa taarifa sehemu husika bila ya kusubiri kusukumwa.

Comments