Friday, October 06, 2006

Mambo ya mgawo hayo



Mpitanjia akipita kwa uangalifu katika jenmereta zinazofua umemekuingiza katika maduka yaliyopo mtaa wa Mchikichi Kariakoo jijini Dar es salaam, wateja katika maduka hayo wanadai kuna makelele mengi yanayotokana na jenereta hizo. Unapofika katikati ya jiji unaweza kuliita jiji la Dar es Salaam, jiji la makelele kila mtaa ni tak tak tak !!!!

Dar es Salaam angani



Unapokua angani ukikaribia kutua nchi za wanyonyaji unaona kabisa vijimitaa vimejipanga kama ni barabara unaona na hata ukikaa ghorofani unaiona tofauti hiyo angalia hapa katika picha iliyopigwa na Deus Mhagale namna sehemu hii ya jiji inavyoonekana.

Monday, October 02, 2006

Wamachinga



Mfanyabiashara katika mtaa wa Zanaki akiwa kajishika kicha akisikitika baada la tingatinga la jiji kuanza kubomoa kibanda chake saa 8:30 Usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita katika operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara jijini Dar es Salaam. Picha hii ilipigwa na Edwin Mjwahuzi

Wednesday, September 27, 2006

Tutaosha miguu ya bodi hii ya mikopo hadi lini?

Mheshimiwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Vijana humu nchini tunaipata joto ya jiwe. Kwanza joto ya kwanza ya jiwe ni ya kupata ajira ukiachilia lile la kupata ajira nzuri suala ambalo linaonekana kama vile ni miujiza au bahati au uwe na mtu wa kukupigia debe. Kataeni huo ndiyo ukweli.

Na upatikanaji wa ajira nzuri yenye kulipa ambayo angalau itakusukuma leo, kesho na keshokutwa inabidi uwe na elimu ya juu ambayo kwa kiasi kikubwa hapa kwetu inakimbilia chuo kikuu.

Tangu mwaka 1995 na nyuma ya hapo serikali yetu imekuwa ikifanya mabadiliko makubwa katika utoaji wa elimu ya juu, walianza na awamu ya kwanza ya pili na sasa ya tatu ya mikopo.

Ni mikopo! Mikopo tuu! changia! changia! Sawa hatuwezi kukwepa, lakini hali hii inakwenda tofauti kabisa na hali halisi ya Mtanzania kwani wakati gharama za tuisheni zikikwea juu, kipato cha Mtanzania masikini mvuja jasho ambaye ndo mwenye watoto wengi kinashuka sana tena vibaya.

Na hadithi hii inakuwa chungu zaidi. Wakati tuisheni ikilipuka juu, fedha ya mikopo ya serikali inazidi kuwa finyu na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi wakiwa watoto wa wakulima na wafanyakazi kubeba zigo zito la kulipa tuisheni.

Tumesikia serikali ikijikakamua angalau kuongeza kabajeti ka kusomesha vijana elimu ya juu na hapana shaka kwamba, baada ya mikopo hii watoto wa walala hoi wengi watabakia hoi kweli kweli.

Tuchukulie kwa mfano kulipa deni la mkopo wa kusoma kwa asilimia 10- 15 tu kwa miaka 10, itamaanisha gharama za ulipiaji deni ambao hauko chini ya sh. 15,000 kwa mwezi.

Hii itafanya vijana wengi wanaohitimu elimu ya chuo kikuu kuchagua kutoenda katika ajira zinazolipa mshahara mdogo, licha ya kuwapo tatizo sugu la ukosefu wa ajira. Wanaweza kujishikiza, lakini katu hawatofanya kazi kiufanisi.

Hakuna jinsi kwa hili kwa sababu, bodi ni moja tuu hakuna mbadala, labda kungekuwa na uwezo watoto wa walalahoi wangekimbilia mbadala mwingine huko wangepata mkopo kwa wakati wakaacha kuwekewa mikwara na vijana wakasoma kwa nafasi.

Wimbo huu wa kila siku bodi! bodi! haijafanya hiki au kile mpaka wafuatwe katika ofisi zao wastuliwe kidogo ‘ waoshwe miguu’ , wabembelezwe ndo watoe pesa, unaturudisha nyuma saana unatujengea wasomi wa hovyo wasiokuwa na utulivu wala busara.

Wakati mwingine huwa nakaa kufikiria huenda kuna watu wanakaa wakifurahia wengine wakitaabika. Haipendezi umefikia wakati kuwe na options kwaajili ya watu kwenda huko ili kusudi isielemewe bodi moja tu.

Wednesday, September 13, 2006

Hayawi hayawi sasa yamekuwa

Nasema kumekucha jogoo limekwishawika huku mwananchi tumeshaingia hewani jamani, kwa habari za kitaifa, kimataifa, biashara na michezo na makala zilizosadifiwa na kuandikwa na watu wenye fikrapevu, wenye upeo mpana sana katika maisha ya jamii ya kitanzania unaweza kutupata kwa kubonya hapa tupo katika majaribio na tutaanza rasmi muda si mrefu!!

Tuesday, September 12, 2006

Mzee wa Sumo amerejeaaaa

Jamani nadhani kuna wale ambao mlikuwa mmeshaanza kukata tamaa nakumbuka rafiki yangu Jeff Msangi alisema amechoshwa kuingia mtandaoni na kukuta mipicha au makala za zamani, sasa Mzee wa Sumo karudi waka waka na mapicha kibaooo ya kila aina kuanzia yale ya kitaifa, kimataifa, michezo, burudani na hata mambo mengine utakayohitaji hebu mcheki kwa kubonya hapa

Tanzania imeweza, lakini UN inahitaji mtazamo mpya

Hiki ndo chungu chenyewe cha maamuzi duniani yaani Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa maamuzi yote duniani yanatoka hapa, unaweza kumuona Waziri Asha-rose Migiro kwa mbali akiendesha kikao


MUDA wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unamalizika Desemba mwaka huu huku ikiwa imeweza kufanya mengi yakiwamo ya kuwashangaza hata wakubwa kutoka mataifa makubwa wanaoamini siku zote kwamba hakuna mweusi anayeweza kupanga jambo na kulitimiza.
Katika kipindi kifupi cha miaka miwili tangu Tanzania iwe mwanachama asiye wa kudumu wa baraza hilo kuanzia Septemba, 2004 hasa sasa, imesukuma ajenda nyingi, ikiwamo ya kupitisha azimio la kuhakikisha kunakuwapo amani ya kudumu kwenye eneo la maziwa makuu, kuanzishwa kwa kamati ya kusimamia mchakato wa amani katika nchi zilizotoka kwenye migogoro (PBC) n.k
Siri hiyo ya mafanikio ya Tanzania imemegwa na mwakilishi wake wa kudumu huko UN, Dakta Augustine Mahiga wakati akitoa mhadhara wa wazi katika Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa Kurasini, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Dk Mahiga alisema kuwa pamoja na kufanikiwa kupiga hatua hizo kwa muda mfupi umoja huo (UN) bado unakabiliwa na changamoto kadhaa kubwa. Naiunga mkono kauli hii ya Balozi Mahiga.
Kwa jumla, katika ramani ya dunia, siyo siri kwamba jina la Tanzania limeweza kujitokeza katika kila sehemu wanakotafuta usuluhishi, ingawa changamoto inabakia kwamba pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea, bado umoja huo unahitaji mabadiliko makubwa ili kuweza kukifanya kuwa chombo cha demokrasia na kilicho zaidi karibu na watu wake.
Yupo mwandishi mmoja mheshimika sana Uingereza ambaye usemi wake umenivutia na nalazimika kunukuu unaosema hivi: “Inafurahisha kuchekesha kwamba kifupi cha Umoja wa Mataifa kinabakia kuwa ni UN. Hii inanipa shida na kufikiri kila mara kama kitu hasi .
Kisichosaidia , cha kufikirika. Kisichokuwa na msaada.” Sina mtazamo kama wake, lakini nikiangalia mambo yanavyokwenda Mashariki ya Kati na kwingineko duniani, inanishawishi kukubaliana na mwelekeo wa fikra za mzungu huyu japo sipendi sana kushabikia masuala ya aina kama yake.
Sitaki kujiingiza moja kwa moja katika masuala yanayotokea katika vita kali kati ya Israel na kikundi cha Hezbollah iliyoharibu kabisa miji ya Lebanon na Israel na jinsi ambavyo umoja huo umechukua hatua au kushindwa kufanya hivyo, lakini inanibidi kwa sababu kama taifa mwanachama yanayomkabili Lebanon yaweza kabisa kuitokea nchi yetu.
Hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa yakifanyika katika umoja huo tangu aingie madarakani Katibu Mkuu wake wa sasa, Koffi Annan, lakini wengi wetu tungali tunajiuliza hivi mabadiliko haya yanayolenga katika mambo yaliyopitwa na wakati katika ushiriki wa mataifa wanachama kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndicho kitu pekee tunachokihitaji?
Kwanini Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani wapate fursa ya kutumia kura ya veto katika kupitisha maazimio ambayo hawana hata haja ya kufanya marekebisho?
Kwanini China wawe na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini siyo Tanzania, India au Nigeria eti kwa sababu Tanzania ni sehemu ya ‘koloni’ la Waingereza tangu miaka ile, kwanini Japan na Ujerumani wanatengwa kuingia ndani ya ‘chungu’ sababu tu eti walipigania upande mbaya wakati wa vita kuu ya pili ya dunia?
Hata hivyo, hata kama uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utaongezeka kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea kufanyika ndani ya umoja huo hivi sasa, tunadhani kutakuwa ufanisi katika ulinzi wa amani wa dunia?
Hivi tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo utayari wa kukabiliana na migogoro na mauaji ya watu wengi kama yale ya Rwanda au Bosnia utaongezeka? Inavyoonekana siyo rahisi. Lakini, tunahitaji UN inayoweza kubadilika na kwenda na wakati.

MTUHUMIWA WA “KUFUTA MADENI” YA MIKOPO AKIRI KOSA, AHUKUMIWA KIGOMA

KIGOMA, Septemba 4, 2026 — Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu Nicholaus Komba Mahitana maarufu kama Abdallah Mahimbo baad...