Wednesday, September 27, 2006

Tutaosha miguu ya bodi hii ya mikopo hadi lini?

Mheshimiwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Vijana humu nchini tunaipata joto ya jiwe. Kwanza joto ya kwanza ya jiwe ni ya kupata ajira ukiachilia lile la kupata ajira nzuri suala ambalo linaonekana kama vile ni miujiza au bahati au uwe na mtu wa kukupigia debe. Kataeni huo ndiyo ukweli.

Na upatikanaji wa ajira nzuri yenye kulipa ambayo angalau itakusukuma leo, kesho na keshokutwa inabidi uwe na elimu ya juu ambayo kwa kiasi kikubwa hapa kwetu inakimbilia chuo kikuu.

Tangu mwaka 1995 na nyuma ya hapo serikali yetu imekuwa ikifanya mabadiliko makubwa katika utoaji wa elimu ya juu, walianza na awamu ya kwanza ya pili na sasa ya tatu ya mikopo.

Ni mikopo! Mikopo tuu! changia! changia! Sawa hatuwezi kukwepa, lakini hali hii inakwenda tofauti kabisa na hali halisi ya Mtanzania kwani wakati gharama za tuisheni zikikwea juu, kipato cha Mtanzania masikini mvuja jasho ambaye ndo mwenye watoto wengi kinashuka sana tena vibaya.

Na hadithi hii inakuwa chungu zaidi. Wakati tuisheni ikilipuka juu, fedha ya mikopo ya serikali inazidi kuwa finyu na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi wakiwa watoto wa wakulima na wafanyakazi kubeba zigo zito la kulipa tuisheni.

Tumesikia serikali ikijikakamua angalau kuongeza kabajeti ka kusomesha vijana elimu ya juu na hapana shaka kwamba, baada ya mikopo hii watoto wa walala hoi wengi watabakia hoi kweli kweli.

Tuchukulie kwa mfano kulipa deni la mkopo wa kusoma kwa asilimia 10- 15 tu kwa miaka 10, itamaanisha gharama za ulipiaji deni ambao hauko chini ya sh. 15,000 kwa mwezi.

Hii itafanya vijana wengi wanaohitimu elimu ya chuo kikuu kuchagua kutoenda katika ajira zinazolipa mshahara mdogo, licha ya kuwapo tatizo sugu la ukosefu wa ajira. Wanaweza kujishikiza, lakini katu hawatofanya kazi kiufanisi.

Hakuna jinsi kwa hili kwa sababu, bodi ni moja tuu hakuna mbadala, labda kungekuwa na uwezo watoto wa walalahoi wangekimbilia mbadala mwingine huko wangepata mkopo kwa wakati wakaacha kuwekewa mikwara na vijana wakasoma kwa nafasi.

Wimbo huu wa kila siku bodi! bodi! haijafanya hiki au kile mpaka wafuatwe katika ofisi zao wastuliwe kidogo ‘ waoshwe miguu’ , wabembelezwe ndo watoe pesa, unaturudisha nyuma saana unatujengea wasomi wa hovyo wasiokuwa na utulivu wala busara.

Wakati mwingine huwa nakaa kufikiria huenda kuna watu wanakaa wakifurahia wengine wakitaabika. Haipendezi umefikia wakati kuwe na options kwaajili ya watu kwenda huko ili kusudi isielemewe bodi moja tu.

1 comment:

NDABULI said...

Haya mabadiliko ya Elimu ambayo kimsingi yalitakiwa yawe mabadiliko ya kutoka kubaya kwenda kuzuri kwa jamii yamekuja na swala la kisiasa ndani yake ambayo yanaleta matokeo ya kugawa mamlaka na rasilimali. Kimsingi tunatakiwe tujue kuwa serikali yetu ina maana gani kuhusu elimu.Maana hii ndio dira ya utaratibu gani wa kuwapatia elimu watu ufuatwe,nadhani ni wakati muafaka kwa jamii kulijadili hili suala na sio la kuwaachia wataalamu tu.