Thursday, July 19, 2007

Askofu Mkuu KKKT



ASKOFU Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, jana amechaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) baada ya kuwabwaga kwa kura nyingi maaskofu wawili, Dk Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Dk Oldenberg Mdegela wa Iringa.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira, aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Mkutano huo, Askofu Martin Shayo, alisema Askofu Malasusa alishinda baada ya kupata kura 132, akifuatiwa na Dk Mdegera ambaye alipata kura 35, huku Dk Munga akipata kura 17.

Awali askofu Shayo alisema mshindi wa uchaguzi huo alitakiwa apate kura theluthi tatu ambazo ni 123 kati ya wapiga kura 184.

Hata hivyo, awali kabla ya uchaguzi huo, kuliibuka hoja kadhaa baada ya aliyekuwa Msimamizi mkuu wa mkutano huo wa uchaguzi, Ibrahim Kaduma, kutangaza kuwa idadi ya wapiga kura walikuwa 216.

Hoja hiyo ilipingwa na na baadhi ya maaskofu na hivyo kulazimika kupiga kura kwa makini na safari hii watu wakipiga kura kwa majina kwa kila dayosisi.

Awali jana asubuhi, kuliibuka malumbano kadhaa kutokana na baadhi ya wajumbe kupendekeza kuwa wagombea ambao waliwahi kushindwa awali kwa kushindwa kupata kura zaidi ya theluthi moja, waenguliwe. Bonyeza hapausome Mwananchi kwa taarifa za kina zaidi. Au unaweza kumtembelea Mpoki Bukuku aliyeipiga picha hii kwa kubonyeza hapa

No comments: