Monday, December 08, 2025

HESLB NA ADAPT IT ZAINGIA MAKUBALIANO RASMI









Dar es Salaam, Jumatatu, Disemba 08, 2025

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeingia katika hatua nyingine ya mageuzi ya kidijitali baada ya kuingia makubaliano rasmi na kampuni ya kimataifa ya TEHAMA, ADAPT IT ya Afrika Kusini, yenye uzoefu mpana katika kuendeleza mifumo ya elimu na fedha barani Afrika. 

Hafla fupi ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika leo, tarehe 8 Desemba, 2025 katika ofisi za HESLB kanda ya pwani, zilizopo jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi kutoka pande zote mbili.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu ili kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa taarifa. HESLB kwa miaka kadhaa imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kidijitali ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaoomba mikopo, mahitaji ya uwazi wa taarifa na kuimarisha mifumo ya urejeshwaji mikopo kwa wahitimu.

Kupitia ushirikiano huu, ADAPT IT itasaidia HESLB kuboresha mifumo ya kiteknolojia, kuboresha mifumo mipya inayowezesha urahisi wa kupata taarifa na kuboresha miundombinu ya usalama wa data. Hii ni hatua muhimu katika kulinda taarifa nyeti za wanafunzi na wahitimu, sambamba na kuboresha kasi ya utoaji huduma bora.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesisitiza kuwa uhusiano huo ni sehemu ya mkakati wa Bodi katika kuhakikisha huduma za mikopo zinatolewa kwa ufanisi zaidi, kwa kuzingatia kuwa ADAPT IT wana uzoefu mkubwa katika elimu ya juu wa kutoa huduma kwa nchi zaidi ya 41 duniani.

 “Tunaamini kwamba teknolojia ni msingi wa utoaji huduma bora... Ushirikiano huu na ADAPT IT utatuongezea uwezo wa kuhakikisha tunatoa huduma bora na kwa wakati, kupitia kufanya maboresho ya mifumo yetu kuwa ya kisasa zaidi, salama na rafiki kwa watumiaji”, amesema Dkt. Kiwia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji ADAPT IT Bw. Luxolo Rubushe, amesema kuwa wako tayari kutoa utaalamu, uzoefu na ubunifu utakaowezesha HESLB kupata mifumo yenye viwango vya kimataifa. “Tunashirikiana na vyuo mbalimbali katika nchi kama Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Namibia, Lesotho, Botswana, Ghana na nyingine nyingi ndani na nje ya bara la Afrika. 

Tupo tayari kushirikiana na HESLB kuleta mageuzi chanya kwa kutumia teknolojia. Ushirikiano wetu na HESLB ni fursa ya kushirikiana katika kuboresha huduma za mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na kusimamiwa nchini Tanzania,” amesema Bw. Rubushe.

Makubaliano hayo yanajikita katika maeneo muhimu yafuatayo:

* Kukuza ushirikiano kati ya HESLB na ADAPT IT kupitia majukwaa ya kidijitali kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa mikopo ya wanafunzi na uzingatiaji wa taratibu.

* Kutambua na kutekeleza shughuli za pamoja kama vile kampeni za uhamasishaji, suluhisho za kiteknolojia na kujenga uwezo kwa watumishi, na

* Kujifunza kuhusu fursa za ADAPT IT katika kupata suluhisho za teknolojia na kusaidia ajenda ya HESLB ya mageuzi ya kidijitali.

Kupitia makubaliano haya, HESLB inatarajia kuongeza ufanisi wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuongeza kiwango cha makusanyo ya mikopo na kupunguza changamoto zinazotokana na ucheleweshaji wa taarifa au mifumo kukwama. Wanufaika wa mikopo, waajiri na wadau wengine pia watanufaika na mifumo iliyoboreshwa ambayo itawapa uwezo wa kufuatilia taarifa muhimu kwa urahisi.

Makubaliano kati ya HESLB na ADAPT IT ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali ndani ya sekta ya elimu ya juu nchini Tanzania. Ni hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali katika kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi.

KAMPUNI YA NOBLE HELIUM KUTOA AJIRA MPYA 50 KUPITIA UTAFITI WA HELIUM KINAMBO




Rukwa

Kampuni ya Noble Helium kutoka Australia imetangaza mpango wa kuajiri zaidi ya vijana 50 kupitia utafiti mpya wa Helium unaotarajiwa kuanza mwezi Desemba hadi Februari katika kijiji cha Kinambo, Wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Akizungumza kupitia mahojiano maalum hivi karibuni Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Pius Simeon Mwita, alisema Noble Helium imefanikisha tafiti mbalimbali za awali na kubaini viashiria muhimu vya uwepo wa gesi ya Helium, huku ikichangia ajira na maendeleo kwa jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji.

Mwita alisema katika tafiti zilizopita kampuni ilitoa ajira zisizo rasmi zipatazo 450, na pia ilishirikisha wananchi kwenye utoaji wa huduma kama ulinzi, usambazaji wa bidhaa, vilainishi kwa shughuli za uchorongaji, zabuni ndogo, ununuzi wa chakula pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Aidha, alisema Noble Helium imekamilisha tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopo katika maeneo ya leseni ya utafiti wa Helium, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha shughuli za kampuni zinaendeshwa kwa kuzingatia maslahi ya jamii na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Mwita, utafiti mpya utakaofanyika Kinambo utaongeza nafasi nyingine zaidi 50 kwa vijana, na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo. 

“Tunawaomba vijana wajitokeze kwa wingi pindi fursa hizi zitakapotangazwa. Lengo letu ni kuhakikisha jamii inanufaika moja kwa moja na uwekezaji huu,” alisema.

Utafiti huo unatarajiwa kuongeza kasi ya maandalizi ya uwekezaji mkubwa wa Helium nchini, gesi ambayo imekuwa na mahitaji makubwa duniani kwa matumizi ya teknolojia za tiba, anga na vifaa vya sayansi.

Waziri Kombo aongoza kikao cha wizara mbili za Tanzania na Balozi wa China










Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Kombo (Mb.) amefanya kikao kazi na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian pamoja na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 6 Desemba 2025.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika  utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kampuni za China ikiwemo miradi ya ujenzi wa barabara, majengo pamoja na viwanja vya michezo na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano kwa siku za mbeleni.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kombo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa ushirikiano wake katika kuimarisha diplomasia ya uchumi na Tanzania kupitia miradi ya maendeleo katika sekta za ujenzi, ikiwemo ujenzi wa Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika mkoa wa Dar es Salaam na ujenzi wa majengo ya Serikali jijini Dodoma.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega ameishukuru China kwa mchango wake katika kutekeleza miradi ya ujenzi nchini, na kusisitiza umuhimu wa kampuni za ujenzi kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati ili kuruhusu utekelezaji wa miradi mipya ijayo, katika muda uliopangwa.

Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ameipongeza China kwa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa mataifa hayo mawili kupanua wigo wa ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wao na vizazi vijavyo.

Awali, Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, amepongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuwezesha utoaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, jambo lililochangia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa

Sunday, December 07, 2025

Tanzania Yaibuka Kidedea kwenye Tuzo za Utalii Duniani








Tanzania imeendelea kushikilia nafasi yake ya kimataifa kama “Nchi Inayoongoza Duniani kwa Utalii wa Safari” katika Hafla ya Fainali za World Travell Awads 2025.

Tanzania imetunukiwa taji hili adhimu katika Sekta ya utalii duniani wakati wa Hafla ya 32 ya World Travel Awards (WTA 2025), iliyofanyika katika Ukumbi wa Exhibition World Center nchini Bahrain tarehe 6 Desemba 2025.

Tuzo za WTA, zinazotajwa kama “Tuzo za Oscars za utalii duniani” kutokana na hadhi yake kubwa katika Sekta, Tuzo hizi zimewaleta pamoja zaidi ya washiriki 500 wakiwemo viongozi wa Serikali na wadau wa utalii.

Tanzania imeshinda Tuzo nne miongoni mwao ni Kisiwa mashuhuri cha Zanzibar (Spice Islands) kushinda Tuzo ya World MICE Awards 2025 kama “Eneo Bora Afrika kwa Mikutano na Matukio ya Kitaasisi.”

Halkadhalika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, imetangazwa kuwa “Hifadhi Bora ya Taifa Duniani 2025” katika tuzo hizo za WTA.

Aidha, Tanzania imepata tuzo mbili zaidi katika kundi la Sekta Binafsi, ikiwemo “Kampuni Bora ya Safari za Puto Duniani,” iliyotwaliwa na kampuni ya Serengeti Balloon Safaris.

Tuzo nyingine imekwenda kwenye Kisiwa bora cha Mapumziko Duniani na Jumaira Thanda Resort katika Kisiwa cha Mafia nchini Tanzania imeibuka mshindi katika kipengele hicho.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo za WTA, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania pamoja na sekta binafsi katika kukuza utalii endelevu na kuimarisha uhifadhi nchini.

Tanzania, ambayo imeshinda tuzo kwa mwaka wa pili mfululizo, inatarajiwa kuwa mwenyeji wa hafla ya fainali ya World Travel Awards itakayofanyika Desemba 2026.

Thursday, December 04, 2025

RC ARUSHA APOKEA UJUMBE WA MABUNGE DUNIANI (IPU)

 






. Kufanya Mkutano wa Mabunge Mkoani Arusha 

.Wajumbe zaidi ya 1500 kutoka nchi wanachama wa IPU kuhudhuria 

. Rais Dkt. Samia apendekezwa kuwa Mgeni rasmi 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Gabriel Makalla mapema leo Alhamisi Disemba 04, 2025  ameupokea na kuzungumza na Ujumbe wa Umoja wa Mabunge duniani (IPU), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano mkubwa wa Mabunge unaotarajiwa kufanyika Mkoani Arusha na kuhusisha Maspika, Wabunge na Viongozi zaidi ya 1500 kutoka kote duniani.

Ujumbe wa IPU umeongozwa na Balozi Ande Filip, akiongozana na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa Geneva,Uswisi Dkt. Hoyce Temu ambapo katika maelezo yake Balozi Ande amesema katika Mkutano huo, Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

"Tanzania ni Mwenyeji na sababu kubwa ni ushiriki na historia yake katika IPU na kikubwa zaidi ni namna wao wanavyoiona Tanzania na sisi tumewahakikishia tupo tayari kuwapa ushirikiano kufanikisha mkutano huo mkubwa wa Kihistoria." Amesema Mhe. Makalla.

Mhe. Makalla amesema Mkutano huo ni fursa kwa Wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla na ukija wakati mzuri katika kudhihirisha amani, usalama na utulivu uliopo nchini na kuaminika kwa Tanzania Kimataifa, akiwataka wananchi kujiandaa kutumia fursa za ujio wa mkutano huo kiuchumi.

Kwa Upande wake Balozi Ande kwaniaba ya Maafisa wengine wa IPU, amesema Mkutano huo wa Kimataifa utafanyika kwa siku sita Jijini Arusha na kulingana na ratiba, washiriki wake kutoka kote duniani watakuwa na zaidi ya siku sita Mkoani Arusha ili kuwapa fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria na Vivutio vya Utalii vilivyopo Arusha na maeneo mengine ya jirani.

Tuesday, November 25, 2025

TUZINGATIE UTU, SHERIA NA HAKI KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA ULINZI WA RASILIMALI ZA TAIFA- DKT KIJAJI

 








Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt Ashatu Kijaji (Mb) amewataka watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuzingatia utu, sheria na haki katika utekelezaji wa majukumu ya ulinzi wa rasilimali za Taifa.

“_Sisi watumishi wa umma tunapaswa kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka na kwa viwango huku tukizingatia haki, sheria na utu wa wananchi tunaowahudumia_” amesema Dkt. Kijaji. 

Mhe. Dkt. Kijaji ameyasema hayo, leo Novemba 24,2025, katika ziara yake ya kwanza ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kujifunza, kujionea jinsi shughuli za uhifadhi na utalii za TAWA zinavyofanyika na kujitambulisha kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Pia, Dkt. Kijaji amesisitiza kuendelea kuimarishwa kwa ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo ya hifadhi kwa kuongeza ufanisi katika doria, ujenzi wa vituo vya askari na matumizi ya teknolojia kama ndege nyuki (drones) na visukuma mawimbi (GPS Collars).

Sambamba na hayo, Mhe.Dkt. Kijaji amezindua vitendea kazi ambavyo ni magari (4) ya shughuli za doria, pikipiki (33) kwa ajili ya shughuli ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na pikipiki ya miguu mitatu (Bajaji) iliyokabidhiwa kwa Askari wa Uhifadhi, Elihuruma Rashid aliyepata changamoto za kiafya akiwa katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande (Mb) amesema kwamba, vitendea kazi hivi vilivyozinduliwa leo ni jitihada zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya wanyamapori.

Kwa upande wake, akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema kuwa Bodi itahakikisha kuwa maelekezo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa ubunifu na weledi wa hali ya juu.

Aidha, Mej. Jen (Mstaafu) Semfuko ameongeza kuwa TAWA itaendelea kuhakikisha kuwa jamii zinazopakana na hifadhi zinafaidika kutokana na rasilimali zilizopo katika maeneo hayo.

Awali, akimkaribisha Mhe. Dkt. Kijaji, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange amesema TAWA ina jukumu kubwa la kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa katika maeneo yanayoisimamia yakiwemo Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu hivyo kuongezeka kwa vitendea kazi hivi kutachagiza ufanisi wa shughuli za doria katika maeneo mbalimbali.

Kadhalika, Kamishna Kabange ameongeza kuwa jitihada mbalimbali zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii zimeweza kuongeza idadi ya watalii kutoka katika mataifa ambayo awali yalikuwa hayana idadi kubwa ya wageni.

“_Jitihada hizi za Mhe. Rais zimewezesha TAWA kupata kampuni ya mwekezaji wa kwanza kutoka Nchini China aliyewekeza katika shughuli za uwindaji wa kitalii,_” amesema Kamishna Kabange.

Katika ziara hii, Mhe. Kijaji aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, Katibu Mkuu wa Wizara ya Malisili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi na Viongozi wengine wa Wizara ya Malisili na Utalii.

MAKAMU WA RAIS NCHIMBI AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI MKUU WA SLOVAKIA KANDO YA MKUTANO WA AU-EU




Luanda, Angola —
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Slovakia, Mhe. Robert Fico, pembezoni mwa Mkutano wa 7 wa Viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya (AU–EU Summit) unaoendelea jijini Luanda.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wamejadili maeneo mapana ya ushirikiano kati ya Tanzania na Slovakia, ikiwamo:

  • Kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi

  • Uwekezaji katika viwanda, teknolojia na miundombinu

Mazungumzo hayo yametajwa kuwa sehemu muhimu ya mkutano huo mkubwa unaolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya, hususan katika maeneo ya maendeleo ya kiuchumi, uwekezaji na usalama.

Makamu wa Rais Nchimbi amepongeza uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Slovakia na kusisitiza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuendeleza diplomasia ya uchumi, kuvutia uwekezaji na kupanua masoko ya nje kwa bidhaa na huduma za Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Robert Fico ameonesha utayari wa Slovakia kuongeza ushirikiano na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa Afrika Mashariki kama kitovu kinachokua kwa kasi katika uwekezaji na biashara.

Mazungumzo hayo yamefanyika wakati viongozi kutoka mataifa mbalimbali wakikutana kujadili mustakabali wa mahusiano ya AU na EU, maendeleo endelevu, amani na ushirikiano wa kimataifa.

#Tanzania #DiplomasiaYaUchumi #AUEUSummit #Luanda2025 #EmmanuelNchimbi #RobertFico #UshirikianoWaKimataifa

ENG. SAMAMBA ASISITIZA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI

  *Afungua Rasmi Maonesho ya 10 ya Madini, asisitiza Ushiriki wa Kampuni za Kizawa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amef...