Ushirikiano wa biashara, uwekezaji, nishati, teknolojia na Akili Unde (AI) kuwa ajenda kuu za mkutano huo.
Dodoma, Oktoba 27, 2026. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameelekea Moscow nchini Urusi kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Afrika na Urusi, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 hadi 29, 2026.
Mkutano huo wa kimataifa unatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa nchi za Afrika na Urusi, ukiongozwa kwa pamoja na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Burundi, รvariste Ndayishimiye.
Katika mkutano huo, viongozi watajadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Afrika na Urusi, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, sayansi na teknolojia, nishati, usalama wa chakula, mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya Akili Unde (AI).
Moja ya mambo muhimu yanayotarajiwa kujadiliwa ni nafasi ya teknolojia na Akili Unde katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, sambamba na kupanua fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili.
Aidha, mkutano huo unatarajiwa kupitisha Tamko la Pamoja na Mpango wa Kazi wa Ushirikiano kati ya Afrika na Urusi kwa kipindi cha mwaka 2027 hadi 2029, ambao utaweka mwelekeo wa utekelezaji wa makubaliano na vipaumbele vya ushirikiano katika miaka mitatu ijayo.
Matokeo mengine yanayotarajiwa ni kusainiwa kwa nyaraka mbalimbali za kiserikali na mikataba ya kibiashara, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Afrika na Urusi.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unatoa fursa ya kushiriki majadiliano kuhusu maeneo muhimu ya ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo uwekezaji, teknolojia na maendeleo endelevu.
Taarifa kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Oktoba 27, 2026.
#MwiguluNchemba #RaisSamia #Tanzania #RussiaAfrica #Uwekezaji #Diplomasia #Teknolojia


.jpeg)

No comments:
Post a Comment