
WAKATI ikiwa zimebaki siku mbili zipigwe visiwani Zanzibar heka heka zimeendelea huku pande mbili zinazovutana kuhusu kura hizo upande mmoja ukiwataka wananchi kutokubali kufitinishwa na kwa sababu za tofauti za kiitikadi kisiasa juu ya uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa na mwingine ukiipuuza.
Upande unaounga mkono kura hiyo umetoa ushauri jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Watu sita ya Baraza la Wawakilishi inayofuatilia kura za maoni, Ali Mzee Ali alisisitiza kura ya ndiyo ni muhimu alipokuwa akizungumza na wananchi mbalimbali katika kikao kilichoanza jana kisiwani humo.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa Madiwani na Masheha wa Mkoa wa Kusini Pemba jana Ali Mzee alisema kwamba hivi sasa kumeundwa utaratibu mmoja wa kuzika siasa za fitina, chuki na hasama ambazo zinahitaji kuepukwa kabisa na badala yake kujenga mustakabali mpya wenye matumaini wenye kuzingatia umoja na mshikamano kwa jamii.
“Nawasihi msikubali kufitinishwa mkapoteza watu wazuri kama ilivyotokea huko nyuma, nadhani nyote mnajua nini kilitokea kwa hivyo nasema tena nakuombeni sana msikubali kurudi katika balaa, tunahitaji umoja na amani zaidi kwa hivyo ni matarajio yangu kuwa mtatumia busara katika kupiga kura ya maoni kuchagua jambo jema na sio kurudi katika vurugu,” alisema Mwenyekiti huyo.
Wakati hayo yakiendelea baadhi ya watu wamekuwa wakisambaza mabango na baadhi ya vipeperushi wakipinga kura hizo za maoni Mjini Unguja. Bango limebandika katika maskani ya kaka ya Mwembe Kisonge ambayo ni kambi ya mmoja wa wagombea kila siku huwa kunaandikwa ujumbe unaofanana 'wana CCM Mseto ni hatari, kura ya maoni tia hapana.'
Mzee alisema Zanzibar hakuna upinzani bali kuna chuki na uhasama mkubwa miongoni mwa wananchi wa Unguja na Pemba hali ambayo inahtaji kurekebishwa na kuondolewa kabisa.
Alisema chaguzi zote zilizofanyika Zanzibar kuanzia Uchaguzi wa kwanza wa 1957 na zilizofuatia zilitawaliwa na vurugu na hata baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ushindani ulikuwa karibu sawa kwani katika matokeo ya Uchaguzi wa 1995 CCM ilishinda Viti 26 na CUF viti 24, lakini nchi haijatulia kabla na baada ya mapinduzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa akizungumza katika mkutano huo, alisema Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalifanyika kuleta hali za watu sawa na kuondoa aina yoyote ya ubaguzi ambapo Afro Shiraz Party (ASP) hakikuwa na dhamira ya kuwafanya Waafrika kuwa juu ya watu wengine hivyo yanayotokea sasa ni kinyume na dhamira ya mapinduzi.
Aidha alisema Kisiwa cha Pemba kimepita katika kipindi kigumu sana cha kususiana mambo mbalimbali, vitendo vya kuhujumiana kuchomeana nyumba, kumwagiana tindikali mwilini na baadhi ya wanaume kuwapa talaka wake zao kutokana na ushabiki wa kisiasa. Imeandikwa na Salma Said. SOURCE:MWANANCHI