Friday, October 03, 2025

ZOEZI LA KUHAMISHA TEMBO TAKRIBANI 500 KUTOKA KYERWA KWENDA BURIGI - CHATO LAENDELEA KUFANIKIWA.












Na. Jacob Kasiri - Kyerwa.

Zoezi la kuhamisha tembo takribani 500 kutoka katika maeneo ya wananchi na mwekezaji wilayani Kyerwa na Karagwe kuelekea Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato linalotekelezwa kitaalam bila adha wala bughudha kwa wananchi na mali zao likiendeshwa na TANAPA kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaendelea kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Tayari makundi makubwa mawili yenye tembo zaidi ya mia moja (100) waliotembea umbali wa zaidi ya kilometa 150 kutoka Kyerwa wameshaingia ndani Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato na kuonesha dalili zote za kutokurudi walipotoka. Hatua hii imekuja baada ya wataalamu wa Ikolojia kutoka shirika hilo kuyafuatilia makundi hayo kwa ukaribu zaidi.

Zoezi hilo linaloendelea kila siku la kuwaswaga tembo kwa kutumia Helikopta mbili (2) za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kwa magari ambapo leo Oktoba 03, 2025 zaidi ya tembo 105 waliokuwa katika makundi mawili (2) wameendelea kuswagwa kutoka Kyerwa yalipo mashamba ya mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari (Kagera Sugar) hadi eneo liitwalo Golini ulipo mpaka wa wilaya ya Kyerwa na Karagwe kuelekea Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato.

Ikumbukwe kuwa Septemba 30, 2025 wakati alipozuru na kushiriki doria ya kuswaga tembo hao, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Massana Mwishawa aliridhishwa na zoezi zima linaloendelea uwandani na alisema;

“Zoezi linaendelea vizuri licha ya changamoto kadhaa zinazojitokeza kwa tembo wakolofi ambao hujitenga na wenzao, pia endeleeni kuyafuatilia yale makundi ambayo mmeshayafikisha hifadhini ili yasirudi tena na kwenda kusababisha karaha kwa wananchi na mali zao japo kwa umbali waliotembea na misukosuko waliyoipata ni vigumu kurudi, ila tuendelee kuwachunguza kwa ukaribu.”

Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyera ACC  Fredrick Mofulu ambaye ndio msimamizi na mratibu wa operesheni hii alisema kuwa watahakikisha tembo wote waliosalia wanahamishwa ili kumaliza kabisa adha waliyokuwa wakiipata wananchi ya kuharibiwa mazao yao na kuhatarishiwa maisha yao na wanyamapori hao.

Sanjari na hilo zoezi hilo pia leo limewahusisha Makamishna Waandamizi wa Uhifadhi ambao ni Charles Ngende - Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Rumanyika - Karagwe na Catherine Mbena, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano - TANAPA. 

Zoezi hili pia limeshirikisha taasisi nyingine za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zikiwemo taasisi za Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mkoani Kagera.

No comments:

Waziri Kombo akutana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika

   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa U...