Tuesday, October 07, 2025

*WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO WIZARA YA MADINI






_⬛Aitaka ifuatilie kampuni zilizoshika maeneo bila kuyaendeleza_

_⬛Aipongeza kampuni ya Huaer International kwa uwekezaji._

_⬛Asisitiza uwekezaji  huo ni utekelezaji wa Maono ya Rais Dkt. Samia_

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini kufanya ufuatiliaji wa makampuni ya madini ambayo yameshilikilia maeneo kwa muda mrefu lakini hawajayaendeleza mpaka sasa yakiwemo makampuni matatu wilayani Ruangwa

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa makampuni ya Nachu, Uranex na Paco Gems Ltd yanapaswa kusema hatma ya maeneo waliyoyahodhi kwa muda mrefu vinginevyo ardhi hiyo itarudishwa kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo leo Jumanne (Oktoba 07, 2025) alipotembelea kampuni ya uchimbaji wa madini Huaer International Limited katika kijiji cha Ng’au Ruangwa mkoani Lindi.

“Kampuni ya Paco Gems tangu 2009 mpaka leo hakuna maendeleo, tunatoka Utanex pale Chunyu, wameshalipa fidia tangu 2012 lakini mpaka leo hii hakuna maendeleo yoyote, ipo kampuni ya Nachu ambayo ilipata heshima ya kusaini mkataba mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpaka leo hii wamepotea na hakuna taarifa.”

Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza kampuni ya Huaer International Limited ambayo imefanikiwa kuanza mchakato wa uwekezaji ndani ya kipindi kifupi baada ya kupata vibali vyote muhimu.

“Kampuni yako ambayo imeanza ukaguzi mwaka 2024, ukapata matokeo mwaka huohuo na kuomba vibali mwaka huohuo, leo mmeanza utekelezaji wa ujenzi na mmefikia hatua hii, ninyi mnapaswa kupongezwa na mnapaswa kuwa mfano wa makampuni haya mengine tata.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa kampuni hiyo ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha ajira kwa Watanzania kupitia uwekezaji. “Kampuni hii ndiyo inaanza na inaendelea na ujenzi mtakapokamilisha mtatoa nafasi ya Watanzania na Wana-Ruangwa kupata ajira hapa.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania waliopata nafasi ya kufanya kazi katika kampuni hiyo kufanya kazi kwa bidii, weledi, nidhamu na uaminifu “Tunahitaji kuwahakikishia hawa wawekezaji kwamba tunaajirika na tunaweza kufanya kazi hizi.

Kwa Upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ameishukuru Serikali kwa kuendelea  kufungua fursa za uwekezaji kwa mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa kichocheo cha maendeleo kwa wakazi wa maeneo hayo.

Amesema kuwa uwekezaji wa kampuni ya Huaer utakuwa ni moja ya fursa kubwa sio tu kwa uchumi wa Wilaya ya Ruangwa au Mkoa wa Lindi bali Tanzania kwa ujumla 

“Sisi upande wa Mkoa tunaendelea kuahidi kutekeleza sera zote za uwekezaji ambazo Serikali inaziweka na kuendelea kushirikiana na wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki ili waendelee kuwa kwa wingi katika mkoa wetu”

Thamani ya mradi huo ni dola za marekani milioni 20.

No comments:

*WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO WIZARA YA MADINI

_⬛Aitaka ifuatilie kampuni zilizoshika maeneo bila kuyaendeleza_ _⬛Aipongeza kampuni ya Huaer International kwa uwekezaji._ _⬛Asisitiza uwek...