Burigi-Chato, Oktoba 4, 2025
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii leo imeendelea na zoezi la kuswaga tembo zaidi ya 100 kutoka maeneo ya makazi ya wananchi kwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi–Chato, katika juhudi endelevu za kudhibiti migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
Zoezi hilo limefanyika kwa uangalizi wa karibu wa maafisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambapo makundi mawili ya tembo waliokuwa wakizunguka katika vijiji vya jirani na hifadhi wamefanikiwa kuswagwa kwa usalama bila madhara kwa watu wala wanyama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na maafisa wanaosimamia operesheni hiyo, tembo hao sasa wako njiani kuelekea Burigi–Chato, wakiwa chini ya uangalizi wa wataalamu wa wanyamapori waliotumia mbinu za kitaalamu, zikiwemo sauti maalum na magari ya kufuatilia mienendo yao ili kuhakikisha wanarejea salama katika makazi yao ya asili.
“Zoezi hili limekuwa la mafanikio makubwa. Tulipokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi waliokuwa wakivamiwa na tembo, kuharibiwa mashamba na wakati mwingine kupoteza maisha. Leo tunashuhudia hatua kubwa kuelekea utulivu na usalama wa kudumu,” alisema afisa mmoja wa TAWA.
Aidha, wananchi wa maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na tatizo hilo wameipongeza serikali kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa imeleta ahuheni na matumaini mapya kwa wakulima na wafugaji waliokuwa wakiishi kwa hofu.
“Tumekuwa tukiteseka kwa muda mrefu, mazao yetu yalikuwa yanaharibiwa mara kwa mara. Tunashukuru kwa hatua hii ya serikali, sasa tunaweza kuendelea na shughuli zetu kwa amani,” alisema mkazi mmoja wa Kagera.
Wataalamu wa uhifadhi wameeleza kuwa uhamisho wa tembo ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu ya kulinda wanyamapori huku ikihakikisha binadamu wanaendelea na shughuli zao bila kuvamiwa. Hatua kama hii inachukuliwa pale ambapo wanyamapori wanatoka nje ya hifadhi kwa sababu mbalimbali kama uhaba wa chakula, maji au mabadiliko ya mazingira.
Kwa mujibu wa TANAPA, Hifadhi ya Taifa Burigi–Chato inatarajiwa kuwa makazi salama kwa makundi hayo ya tembo kutokana na ukubwa wake, upatikanaji wa maji na malisho ya kutosha, sambamba na usimamizi madhubuti wa ikolojia ya eneo hilo.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha doria, elimu kwa wananchi, na uwekezaji katika vizuizi vya kiasili ili kupunguza zaidi migongano ya binadamu na wanyamapori nchini.




.jpeg)

No comments:
Post a Comment