Thursday, October 09, 2025

MSAJILI HAZINA ASHIRIKI UZINDUZI UJENZI MGODI WA MADINI KINYWE

 









Na Mwandishi wa OMH

Mahenge, Morogoro. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ameshiriki uzinduzi wa shughuli za ujenzi wa mgodi wa madini ya kinywe (graphite), uliofanywa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, katika hafla iliyofanyika Alhamisi, Oktoba 9, 2025, katika eneo la Mahenge, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Faru Graphite Corporation, kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (hisa 16%), na Black Rock Mining Limited (hisa 84%), ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya madini nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mavunde alisema ujenzi wa mgodi huo unatarajiwa kugharimu takribani $510 milioni (zaidi ya Sh1.3 trilioni).

Aliendelea kusema kuwa uwekezaji huo utazalisha ajira zaidi ya 400 wakati wa ujenzi na zaidi ya 900 za kudumu mgodi utakapoanza uzalishaji kamili. 

Nje ya mgodi, alisema Mhe. Mavunde, ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 4,500 zinatarajiwa kuchochewa kupitia mnyororo wa thamani wa wachuuzi, wakulima, wasambazaji wa bidhaa na watoa huduma.

Serikali inatarajia kupata zaidi ya $3.2 bilioni (zaidi ya Sh7 trilioni) katika kipindi cha uhai wa mgodi---miaka 26, kupitia kodi, tozo, gawio, na mrabaha wa madini.

“Mradi huu wa ujenzi wa mgodi wa Kinywe ni kielelezo cha kasi mpya katika kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.

“Mradi huu si uchimbaji wa rasilimali pekee, bali ni injini ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara, ajira, na ustawi wa jamii kwa ujumla.”

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Faru Graphite Corporation, alisema Serikali kupitia ubia huu inalinda maslahi ya taifa, ikinufaika kupitia hisa, kodi, ajira na mzunguko wa fedha.

Aliongeza kuwa mradi huo utachangia kuimarisha uchumi wa taifa, kwani sehemu kubwa ya madini itauzwa nje ya nchi, hivyo kuongeza mapato ya kigeni, kuendeleza biashara za ndani, na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi wa eneo husika na mikoa jirani. 

Pia, alibainisha kuwa uwekezaji kama huo unasaidia kuimarisha sekta ya madini na kufanya Tanzania kuwa kitovu cha malighafi za teknolojia safi barani Afrika.

Madini ya graphite ni miongoni mwa malighafi muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki, na paneli za umeme wa jua.

“Tumejizatiti kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kukuza uchumi wa taifa inatimia kikamilifu, hususan kupitia sekta ya madini na uwekezaji wa kimkakati,” alisema Bw. Mchechu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, alionesha furaha yake ya mkoa wake kupata bahati ya kuwa mwenyeji wa miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo wa  Faru Graphite.

“Huu ndio mradi mkubwa zaidi kuwahi kutekelezwa katika Mkoa wa Morogoro,” alisema Mhe. Malima, huku akielekeza wataalamu wa mkoa kuandaa semina zitakazowaelimisha wananchi kuhusu fursa za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na mradi huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Faru Graphite Corporation na Mwakilishi wa Black Rock Mining Limited, Bw. Richard Crookes, alisema kampuni yake imejipanga kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafuata viwango vya kimataifa vya usalama, uhifadhi wa mazingira, na teknolojia rafiki kwa mazingira.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyovutia uwekezaji huu mkubwa,” alisema Bw. Crookes.

No comments:

MSAJILI HAZINA ASHIRIKI UZINDUZI UJENZI MGODI WA MADINI KINYWE

  Na Mwandishi wa OMH Mahenge, Morogoro. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ameshiriki uzinduzi wa shughuli za ujenzi wa mgodi wa madi...