
Timu ya Benki ya ABSA Tanzania ikiwa katika picha ya pamoja kwenye mradi wa Kawe 711 jijini Dar es Salaam.
Tarehe 10 Oktoba 2025, timu ya wataalamu kutoka Benki ya ABSA Tanzania imefanya ziara maalum katika miradi mikubwa ya makazi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam — ikiwemo Samia Housing Scheme – Kijichi na Kawe 711 Housing Project.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuwajengea
uelewa maafisa wa ABSA kuhusu utekelezaji wa miradi ya NHC, kuonyesha fursa za
ununuzi wa nyumba, na kuimarisha ushirikiano katika kusaidia Watanzania
kumiliki makazi bora kupitia mikopo ya nyumba.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ABSA Tanzania, Bw. Obedi Laiser,
ambaye hakuficha furaha yake baada ya kujionea kazi kubwa inayofanywa na NHC
katika kubadilisha sura ya makazi nchini.
“Tumepata
fursa nzuri ya kujifunza na kujionea kazi kubwa inayofanywa na NHC. Nyumba hizi
ni za kisasa, zenye ubora wa juu na zitachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza
changamoto ya uhaba wa makazi nchini. Tunawapongeza NHC kwa ubunifu na ufanisi
mkubwa katika utekelezaji wa miradi hii,” alisema Bw. Laiser.
Aidha, alisisitiza kuwa ubora wa miradi ya NHC
unaendana kikamilifu na falsafa ya chapa ya ABSA inayosema “Hadithi yako ina thamani”, akifafanua kuwa nyumba hizo
zinaakisi maisha halisi ya Watanzania na ndoto zao za kumiliki makazi bora.
Kwa upande wa NHC, Meneja
Miradi, Injinia Grace Musita, aliyeongoza maelezo kwa niaba ya
Shirika, alieleza kuwa miradi ya Samia Housing na Kawe 711 ni sehemu ya
utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“NHC
imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora, salama na ya kisasa.
Miradi hii inajengwa kwa kutumia teknolojia za kisasa, ubora wa hali ya juu na
kwa kuzingatia mazingira rafiki,” alisema Injinia Musita.
Naye Bw.
Deogratious Batakanwa, Meneja wa Mauzo na Masoko wa NHC,
aliishukuru Benki ya ABSA kwa ushirikiano wa muda mrefu katika kusaidia ujenzi
na mauzo ya nyumba za Shirika.
“Tunathamini
ushirikiano wa ABSA kwa kutuwezesha kifedha katika ujenzi wa miradi yetu, na
pia kwa kuwasaidia wateja wetu kupata mikopo ya nyumba. Ushirikiano huu ni
mfano bora wa taasisi za kifedha na sekta ya makazi kufanya kazi kwa pamoja kwa
manufaa ya Watanzania,” alisema Bw. Batakanwa.
Ziara hiyo imetajwa kuwa ni mwanzo wa hatua
mpya ya ushirikiano wa kimkakati kati ya NHC
na ABSA Tanzania, ikilenga
kuendeleza jitihada za kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora,
yenye hadhi na ya gharama nafuu.
Kupitia miradi kama Samia Housing Scheme – Kijichi na Kawe 711, NHC inaendelea kuthibitisha
uwezo wake wa kubadilisha mandhari ya miji ya Tanzania na kuwa nguzo muhimu
katika ujenzi wa Taifa lenye ustawi wa makazi bora kwa wote.
π
NHC – Tunajenga Taifa, Tunakuza Ndoto.
#NHC #ABSA #Kawe711 #SamiaHousing #MakaziBora #UshirikianoWaMaendeleo
#TunajengaTaifa #DarEsSalaam
No comments:
Post a Comment