WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa.
Kutokana na uteuzi huo, tayari Rais Jakaya Kikwete amemruhusu Asha-Rose kwenda kuchukua nafasi hiyo haraka iwezekanavyo, hiyo ikimaanisha kuwa nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sasa imebaki wazi.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jioni ilisema kuwa uteuzi huo umefanywa na Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ambaye amechukua nafasi ya Koffi Annan, akianza kazi hiyo mpya mwezi huu.
Taarifa hiyo imemkariri Rais Kikwete akisema anayo furaha kubwa kwa Mtanzania kupewa nafasi kubwa kama hiyo ya kuutumikia Umoja wa Mataifa ambao ndiyo chombo cha juu kabisa duniani.
"Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni wizara nyeti kwangu, lakini uteuzi huu pia ni heshima kubwa kwa Tanzania na kwa Migoro mwenyewe," ilisema sehemu ya taarifa hiyo, ikimariri Rais Kikwete.
Mapema kabla ya uteuzi huo, Moon alizungumza kwa simu na Rais Kikwete kumweleza juu ya uamuzi wake kutaka kufanya kazi na Waziri Migiro, na yeye mwenyewe akampigia simu Migiro kumjulisha juu ya uteuzi huo.
Wakati akiteuliwa kupewa nafasi kubwa namna hiyo katika Umoja wa Mataifa, Migiro alikuwa hayupo nchini kwani alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Lesotho.
Migiro anakuwa Mtanzania wa pili kupewa wadhifa mkubwa katika Umoja wa Mataifa baada ya mwanamke mwingine, Profesa Anna Tibaijuka, kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Makazi ya Umoja wa Mataifa (UN- Habitat) yenye makao yake makuu Nairobi, Kenya.
Comments