Monday, October 09, 2006

Tunaisubiri semina elekezi ya wamachinga


JAMANI ngoja niseme hata kama mpo wale mtakaochukia, lakini huu ndio ukweli. kwamba, haya masuala ya semina elekezi kila sehemu na kila siku, ipo siku wenye pesa zao watalalamikia!
Haiwezekani, muwe mnakula pesa zetu sote nyinyi tuu, kwa kivuli cha semina elekezi au nini, hivi mnaelekezwa nini hicho msichokijua ambacho kinahitaji kuhama mji na kujificha Arusha! Hivi hamuwezi kuelekezwa kwa njia nyingine kuliko hiyo ya kutumia pesa za kodi zetu nyingi tu na tena wengine wametoka Arusha juzi tu, walikuwa na semina elekezi yao wale ni wataalamu wa Wizara ya Afya kutoka kote Tanzania.
Hawa wameingia na hii staili ya kisasa ya kuchapisha fulana kibao na kofia, hivi hizo kofia na mikoba ndivyo vinavyowafanya muelekezwe kwa urahisi au vipi, mbona mawaziri hawakufanya hivyo, na je hamuoni kwamba mnatumia pesa zetu nyingi hivi hivi tu?
Kama lengo ni kutaka tutekeleze ilani ya chama tawala, CCM, basi hata sisi wamachinga tunaisubiri semina yetu, hasa ya jinsi au namna ya kuendesha vibanda na biashara zetu kwa kasi mpya.
Na siyo wamachinga tu hata wafyeka nyasi, wazoa taka, wazibua vyoo, wajenzi, walimu, wauguzi, polisi, wanajeshi, waandishi wa habari n.k, ipo siku nao wanahitaji uelekezi hivi wote hawa wakijichimbia huko tutabaki na nini?
Mimi nilidhani kuwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuwapiga msasa mabosi kama mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya na kisha kutembelea kila wizara na baadaye katika maeneo nyeti hiyo itatosha, lakini inaonekana bado.
Tunasubiri mlolongo wa semina elekezi zaidi ya 20 kama itakwenda kwa mujibu wa wizara zilivyo na kisha nyingine 26 kama itaenda kwa mujibu wa mikoa na baada ya hapo zaidi ya 126 kama itakwenda kiwilaya.
Na kama hiyo itaendelea hivyo, sijui tuna wilaya ngapi na kisha vijiji vingapi na hatimaye mwisho wa siku mwaka 2010 utakuwa umefika kote huko na hakuna kitakachokuwa kimefanyika. Sisemi hivi kwa sababu nina wivu sana. La hasha!
Natambua kwamba Rais Kikwete kwenye semina elekezi ya Ngurdoto alikuwa na maana njema tu ya kutaka watendaji kutekeleza malengo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tunaweza kusema lengo la semina hizi lengo lake kwa tafsiri nyingine ni kutoa elimu kwa viongozi juu ya namna ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete katika semina elekezi alitilia mkazo suala la ubunifu na kuwa na mawazo mapya na kwamba semina elekezi ya Ngurdoto iwe ni hamasa ya kuwapa mwanga wa kubuni miradi yenye kutekelezeka na faida kwa wananchi.
Suala la msingi ambalo pia Rais Kikwete alilisisitiza ni kuwaelekeza viongozi kutumia yote yanayowezekana kuleta mabadiliko ya haraka katika uchumi wa Tanzania.
Semina elekezi, naamini ilikuwa ni ‘shule’ nzuri kwa viongozi kuwapa chagamoto ya kubadilisha hali ya kila Mtanzania kuwa na neema zaidi.
Zamani wakuu wa sehemu mbalimbali walipokuwa wakiteuliwa hawakuwa na fursa ya kuhudhuria semina elekezi kama ya Ngurdoto, kilichokuwa kikifanyika ni kupewa barua ya maelekezo ya kazi na kuanza kazi mara moja. Wengi walishindwa kutofautisha uongozi wao na utekelezaji wa majukumu kwa mihimili mingine ya dola.
Lakini, kikubwa tunachotaka hapa Watanzania ni kuona matunda ya semina hizo kwa viongozi na kwamba kila kiongozi atajitahidi kuwa na miradi ya maendeleo katika eneo lake. Ni vyema msimamo huo wa Rais Kikwete ukachukuliwa kuwa ni changamoto muhimu ili viongozi wote wa Tanzania wawe na aibu kutangaza kwamba maeneo wanayoongoza yamefanikiwa zaidi kimapato wakati wananchi wengi wa eneo hilo wanagubikwa na umasikini.
Hatutarajii semina elekezi ikawa ni kijiwe cha kuvuna posho kubwa kubwa tu na kisha mambo yakabaki vile vile kama ilivyobainika katika baadhi ya maeneo ya nchi alikoweza kutembelea Waziri Mkuu Edward Lowassa. NawatakiaJumapili njema.

7 comments:

boniphace said...

kaka nimesoma hapa na kugundua usanii ule wa kusema sasa hakuna semina na warsga na kisha kubadili jina na kuziita semina elekezi kisha lengo likawa lile lile la kutafuna posho. Nungana nawe, hakuna jipya wajifunzalo katika semina hizo kama wanataka mafunzo wachukue vitabu wasome na sio kutafuna posho na kusinzia katika hizo wanazoziita semina elekezi, kwanza ni nani anamuelekeza mwenzake wakati wote wanaonyesha kutokuwa na dira na muelekeo unaoweza kupimwa moja kwa moja?

mzee wa mshitu said...

Hahahaa kaka hapa umenifurahisha yaani hii pointi ya dira na mwelekeo hakika ndo hasaa umefika penyewe, wahuni sana hawa watu, wanatafuna pesa zetu hivi hivi tuu!!!

Simon Kitururu said...

Bado nakumbuka semina kadhaa watu walikataa kwenda kisa hakuna posho.Naelewa umuhimu wa posho katika kuwezesha watu waende kwenye semina.Lakini hizi posho vilevile ni tatizo.Semina nyingi watu hawajifunzi kitu , bali huenda kwa sababu wanalipwa posho na kuna msosi mzuri. Naamini bila fikira za hivi kufutika, ni wachache sana ambao wanaelimika katika semina hizi.

mloyi said...

Semina elekezi, jina jipya, lengo lake ni kuendeleza nchi, hivyo wadau muhimu ndiyo wanabidi wapewe hizo semena.
Madaktari, Polisi, mahakama, wauguzi, wazoa taka, wafagia barabara, walimu , wanafunzi nao pia inabidi waandaliwe semina zao, cha kushangaza hawa walio muhimu hawakuandaliwa semina hata moja. wameishia kupewa amri za utekeelezaji wa wajibbu wao bila kujua utaratibu wenye tija kwao.
Sijui makundi ya hapo juu kama yanajua madhara ya rushwa, kutotimiza wajibu wao, mfano sikutatu zilizopita watu wa Ilala na buguruni tulikosa umeme kwa sababu nguzo moja ilianguka, maana kuna kundi halikutimiza wajibu wake mapema.
Naona nao pia wanahitaji semina hizo.

MICHUZI BLOG said...

wakati naungana na kaka makene, mie maoni/ushauri yangu/wangu ni kuwepo pia na semina/warsha/kongamano na nini sijui kwa waandishi wa habari bongo juu ya kutafuta na kuandika (sio kuripoti) habari kwani sasa ingawa inauma lakini ukweli ni kwamba tumeshobokea hotuba za viongozi na vyanzo vya habari vya mezani. sina uhakika kwamba wote tutasinzia kama anavyohofu makene, na kama kitururu kapatia, posho iwepo lakini yenye masharti. aidha wataofanya kazi baada ya kikao ndo walipwe... sijui lakini. ila kweli fani inapotika na imefikia mwandishi kwenda tff ama maelezo ama wizara ama idara fulani ama aliko jk ndo kusaka habari. wananchi tunawasahau.

naomba kuwakilisha

Sultan Tamba said...

Jamani mmesahau ule usemi wa Mzee Ruksa? Yeye alisema hivi: KILA ZAMA NA KITABU CHAKE! Zama za Mkapa aliibuka na kitu kinaitwa TUME, ikawa kila kukicha tunasikia tume mpya! Ishatokea mpaka Wafanyakazi wa shirika moja la Umma walimfuata Mkurugenzi wa bodi kumlalamikia kwamba TUME ZIMEKUWA NYINGI SANA ZIPUNGUZWE ZINAMALIZA PESA. Unajua jibu la Mkueugenzi lilikuwaje? Alisema: TUNATUNDA TUME NYINGINE KUCHUNGUZA PENDEKEZO LENU! Kwa hiyo watu wakala sana kwa kivuli cha Tume.
Zama hivi za Kikwete, yeye amekuja na lake, ambalo ni hili SEMINA ELEKEZI! Kwa hiyo watu nao wanakula kwa kivuli hiki cha SEMINA ELEKEZI! Ndiyo nchi yetu hiyo!

Ndesanjo Macha said...

Unajua huu utamaduni wa mashirika yasiyo ya kiserikali ulipoanza kujishinikiza Tanzania wakati wa kipindi cha mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi, ndio tabia hii ya semina, warsha, makongamano, mikutano inayoendana na posho, chai ya saa nne, chakula cha mchana, chai ya saa kumi, n.k. ulianza. Ndio tabia pia ya waandishi kutoandika kuhusu mikutano hadi mkutano uwe na mshiko. Kuanzia hapo jambo muhimu kwenye mikutano na warsha likawa sio mada na maarifa yatakayotolewa bali kiasi cha mshiko.

Umeuliza swali zuri sana, je wamachinga nao semina yao ya kuendesha biashara ni lini?