Watalii wakiwasili uwanja mdogo wa ndege wa Seronera wilayani Serengeti mkoa wa Mara uliopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Senapa) kwaajili ya kutembelea vivutio vya kitalii wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Serengeti - Idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Senapa) imeongezeka katika siku za hivi karibuni kutokana na sekta ya utalii kukua huku miundombinu ya barabara na viwanja vidogo vya ndege vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo kufanya kazi vizuri.
Afisa Utalii wa Senapa,Evance Magomba alisema kuwa baada ya kujengwa jengo dogo la wageni wanaowasili na wanaoondoka katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera idadi ya wageni imeongezeka huku wakala wa makampuni ya ndege wakiweka wawakilishi wao katika uwanja huo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu kumekua na safari za ndege 3,724 katika uwanja wa Seronera huku uwanja wa Lobo katika kipindi hicho ni safari 349 na uwanja wa Kogatende safari 564.
Alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna viwanja vidogo vya ndege saba kikiwemo cha Seronera ambacho ni kikubwa zaidi chenye uwezo wa kupokea ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 60 ikiwemo ya shirika la Precision Air inayofanya kazi mara nne kwa wiki.
“Miaka miwili iliyopita hatukua na jengo hili la abiria naamini pamoja na sababu nyingine limekua kishawishi kwa wageni kuongezeka kwani linawawezesha kuwa na sehemu nzuri ya kupumzika kabla ya kuanza safari zao,”alisema Magomba
Alisema kutokana na ukubwa wa hifadhi hiyo wanavyo viwanja vingine vilivyosambaa maeneo mbalimbali ili kutoa huduma kwa urahisi na kuwawezesha watalii kupata muda mzuri wa kutembelea vivutio zaidi.
Magomba alivitaja viwanja vingine kuwa ni Kogatenda,Lobo,Ndutu,Kirawira ,Fort Ikoma na Lamai ambavyo hutumika kwa malengo ya kurahisisha kufika eneo husika na kulingana na watalii wanapenda kuona vivutio maalumu.
“Hifadhi ya Serengeti ina uwezo wa kupokea wageni wa aina zote na zipo huduma za malazi zikiwemo hoteli saba,makambi ya kudumu sita na makambi ya muda zaidi 140 yaliyosambaa na kipekee tuwakaribishe wananchi kutembelea hifadhi zetu kwasababu zipo bei maalumu kwaajili yao,”alisema Magomba
Dereva wa kampuni ya kitalii ya Micato Safaris,Emmanuel Lema alisema huduma za kitaalii nchi zimekua kwa kasi baada ya serikali kupitia Bodi ya Utalii(TTB),shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa) na wadau wengine wa utalii kutangaza kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii.
Alishauri Tanapa kuongeza ukubwa wa jengo la wanaowasili na kuondoka na huduma zingine muhimu ili kuwawezesha watumiaji wa jengo hilo kupata huduma za kiwango cha juu hasa wakati wa msimu wa utalii.
Watalii wakiwasili uwanja mdogo wa ndege wa Seronera wilayani Serengeti mkoa wa Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,kukamilika kwa jengo la wageni wanaowasili na wanaondoka kumerahisisha huduma za usafiri ndani ya hifadhi hiyo.
Afisa Utalii Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti mkoa wa Mara,Susuma Kusekwa akizungumza na watalii waliotembelea hifadhi hiyo.
Watalii wakimsikiliza Zacharia Mathayo ambaye ni mwongoza watalii wakati akitoa maelezo kuhusu uhamaji wa wanayamapori aina ya Nyumbu kutoka Kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti hadi Kusini.
Watalii hufurahia kuona wanyama wakubwa wakiwemo Tembo na wengine wanaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Tembo ni mojawapo ya kivutio kikubwa kwa watalii wanaotemebela hifadhi hiyo.
Wanyama wadogo aina ya Pimbi ni sehemu ya vivutio utakavyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Wanyama wadogo aina ya Pimbi ni sehemu ya vivutio utakavyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imefanikiwa kutangaza vivutio vyake kikamilifu sio kwa watalii wanaotoka mataifa ya Ulaya,Asia na Amerika pekee bali pia watalii wa ndani ni sehemu ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.
Makundi makubwa ya Simba kama hili utayaona ndani ya hifadhi hiyo.
Comments