Wednesday, January 10, 2018

NAIBU WAZIRI AWESO AZIAGIZA HALMASHAURI KUTOWAPA KAZI WAKANDARASI WASIOJALI MASLAHI YA TAIFA

 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akitembelea Kijiji cha Mendo, mkoani Shinyanga 
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mendo, mkoani Shinyanga 

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akikagua mtambo wa maji Kijiji cha Mendo, mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, ameziagiza halmashauri zote nchini kutowapa kazi za utekelezaji wa miradi ya maji wakandarasi wasiojali maslahi ya taifa na kusisitiza kuwa Serikali haitavumilia wakandarasi wazembe, ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza kwa muda uliopangwa.

Aweso alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Shinyanga na wakazi wa Kijiji cha Mendo, mkoani Shinyanga na  kusikitishwa na mwenendo wa utekelezaji usioridhisha wa mradi wa maji kijijini hapo.

‘‘Nikuombe sana Mkurugenzi wa Halmashauri, hakikisha mnawapa kazi wakandarasi watakaohaikisha miradi inakamilika kulingana na mikataba yao, miradi mingi ya Serikali imekua haina manufaa kwa wananchi na kukosa tija kwa taifa kwa sababu tunawapa wakandarasi wazembe, wanaokosa uzalendo na kutokujali maslahi ya taifa.’’

‘‘Mfano mzuri ni mradi huu wa Mendo ulioanza kutekelezwa tangu Aprili 2014 na ulitakiwa kukamilika Disemba 2017, lakini bado haujakamilika wakati Serikali imeshaingia gharama ya zaidi ya Sh. mil 300. Jambo ambalo si sahihi, hivyo naagiza ifikapo mwisho wa mwezi huu uwe umeshakamilika na wananchi wapatao 2199 waanze kupata maji,’’ aliagiza Naibu Waziri Aweso.

Naibu Waziri Aweso ameanza ziara ya siku 5 mkoani Sinyanga inayolenga kukagua maendeleo ya miradi ya maji na kuweka msukumo katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa nia ya kuhakikisha inakamilika kwa wakati na wananchi wa  mkoa huo wanapata huduma ya maji  ya uhakika kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Post a Comment