Wednesday, May 03, 2006

Takrima chali, bado zingine ili kustawisha demokrasi

WIKI iliyopita ile sheria angamizi iliyoanza kijichimbia mizizi, iliyokuwa nia ya kuingiza wakora na matajiri madarakani na kuzuia kabisa haki na nafasi ya walalahoi kupata nafasi za uongozi, takrima, ilitupiliwa mbali.

Sheria hiyo iliyokuwa na nia na madhumuni ya kuwapora wananchi uhuru wa kuchagua viongozi kwa utashi wao, na kuwazuia kuhoji uporaji huo, kutokana na kuweka masharti magumu ya kuhoji njia ya kujipatia madaraka hayo ya uwakilishi.

Hii ni sheria nayothubutu kuiita ya ajabu ajabu ambayo chama tawala iliiunda kwaajili ya kujilindia maslahi yao kwa madai eti inaendana na ukarimu na utamaduni wa Watanzania.

Hivi nani asiyejua kwamba kwa mujibu wa desturi za Kiafrika, mwenyeji huwa ndiye mwenye wajibu wa kuwakirimu wageni na sio mgeni kukirimu wenyeji, sasa ilikuwaje mpaka hawa watunga sheria wakajipangia utaratibu huu dhalimu!

Mgeni kukirimu mwenyeji siyo kawaida sana (ukiacha ndugu, jamaa na marafiki), ingawa imeanza kujiotesha mizizi siku za karibuni. Ni rushwa.

Sheria yenyewe iliyotupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Tanzania, ni inayohusu vifungu vya 119(2) na 119(3) vya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kama ilivyorekebishwa mwaka 2000 vinavyoruhusu matumizi ya takrima katika uchaguzi.

Mahakama ilifikia uamuzi huo kwa kuwa vifungu hivyo vinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.

Hakuna kati yetu (labda watoto wadogo) ambaye hajashuhudia namna serikali zilivyojibadili, badala ya kuwa watetezi wa wanyonge na au wajenzi wa taifa, wakabadilika na kuwa wakandamizaji wa raia na waliopenda kujitajirisha wenyewe. Na wakatamani kubaki hivyo milele.

Ukarimu wa kupeana chumvi, kanga , vitenge na pombe na kisha kuyapeleka kiupogoupogo maisha ya watu hao kwa miaka mingine mitano!

Ukarimu wa kujidai kuoneana huruma wakati wa kutafuta ulaji, na mkishaingia katika chombo cha kutunga sheria mnakaa kimya, wengine hata miaka mitano! Hivi hamna namna ya kukarimu wenzenu? Kwanini isiwe wakati wa shida.

Wengine wakishamaliza ‘ukarimu’ wao huo wanahama kabisa majimbo yao kwa miaka mitano na kisha kujificha Dar es Salaam na Dodoma na inapofika miaka mitano wanarejea ‘ukarimu’ wao huo.

Tunaweza tukawa angalau tumevuta pumzi wapenda demokrasia, lakini bado kuna sheria nyingine ambazo zinaendelea kuturejesha kulekule, mathalani sheria ya uchaguzi inayokataza ugombea binafsi.

Itakosa nini ikiruhusu wagombea binafsi zaidi ya kupata faida, kwanza malalamiko yatapungua, lakini pili wananchi wasio na upenyo wa kugombea watapata fursa ya kuitumia haki yao ya kidemokrasia.

Hivi tutakosa nini au serikali ambayo iko chini ya chama tawala itabadili sheria na mfumo mzima wa uchaguzi ambao unachochea tabia chafu kama rushwa.

Au pia tutakosa nini tukirekebisha sheria za usajili wa vyama kuwa huru kuungana ili kusudi wakichoshwa na CCM wanaunda umoja wao chap chap na kisha wanashinda. Hapa sina maana miunganiko kama ile ya Kenya la hasha namaanisha miungano endelevu.

Kama Tanzania tunataka kustawi, tunatakiwa kuondokana na dhana za kujiona sisi ni bora kuliko wengine kwani wapo wengi wanaweza kutenda au kuendesha nchi vyema kuliko sisi.

Cha msingi pia kwa upande wa wananchi ni kubadili mitazamo, fikra, desturi ili hata akija tajiri wananchi tuwe tumejiandaa kisaikolojia kukataa rushwa ya chumvi na kanga kwa mustakabali mwema wa taifa letu.

5 comments:

John Mwaipopo said...

Mwaka 1995 nilikua kwenye mkutano wa mgombea mmoja wa chama cha upinzani. Niliporejea nyumbani nikaulizwa na bibi mkubwa "Vipi umeleta nini kutoka huko kwenye kampeni?" Nafikiri alikuwa anauliza kuwa badala ya kufanya shugulu zingine nilifuata nini mkutatoni ninakojua hakuna 'kitu'

Huu ndio utamaduni duni na dhalimu tuliojijengea miaka ya karibuni. Cha kuchekesha tukapitisha iwe sheria halafu tukacheka na kuchana mbavu.

Majaji wa mahakama kuu nao wana swali la kujibu hapa. Walikuwa wapi siku zile hata wakakaa kimya. Au waliogopa kunyang'anywa mashangigi. Hata kama hawahusiki na uundaji na upisishaji wa sheria kwa nini walikaa kimya badala ya kuiamsha jamii kuwa haki zake zinabakwa na watunga sheria wa Dodoma.

Kati ya mambo uliyoainisha, pia litazamwe la kubuni ama kutunga sheria ama kanuni yakumtaka mwakilihsi wa pahala fulani kuwapo jimboni kwake phisically (kiwahili cha 'phisically'?) walau kwa asilimia fulani ya utumishi wake.

Niliwahi kusoma katuni ya kipanya iliyomuonyesha spika akiwatakia kila la heri wabunge kurejea majimboni kujua matatizo ya wananchi. Mheshimiwa mmoja akang'aka "Majimboni wapi bwana. Mambo yote Daslam 'ikipinda itoe' halafu majimboni"

Hao ndio wawakilishi wetu. Lakini na sisi wananchi tumekuwa mazuzu mno kuwarejesha mara kwa mara. Kuna mtu mmoka anaitwa Mungai na mwingine mzindakaya na wengine wengi tu. Wamekaa sana majimboni mwao. Wao ni god-bestowed lot? Kasheria kengine ka maximum miaka 20 am 15 kanahitajika hapa

Alamsik Binuur

boniphace said...

Mzee wa Mshitu naungana nawe kuhusu agenda ya wagombea binafsi. Niliwahi kuishupalia na kisha kuiweka kando nadhani nitatulia na kupanda na makala za aina hiyo baadaye kidogo. Kinachotakiwa ni kuendeleza vita hivi maana hata hiyo takrima imefutika baada ya kuitwa sana rushwa ambayo imeidhinishwa Tanzania na sio vinginevyo.

mzee wa mshitu said...

Mwaipopo umenikumbusha kitu kuna majamaa wengi mpaka leo hii hawaichukulii kampeni kama mpango wa kutangaza sera na kujinadi kwa mipango makini, wanachukulia kama wakati wa kuvuna.
Nakumbuka mwaka jana wakati wa zile kampeni za awali katika kura za maoni za CCM nimeshuhudia binafsi watu kama wanane au tisa ambao walifika kwangu binafsi wakitaka wapakwe mafuta kwa jamii eti iwaelewe vyema wao hawa walimwaga takrima, walitumia pesa nyingi, lakini mwisho wa siku hawakupata kitu kwa hiyo mpango huu ulikuwa unafaidisha wazembe wachache na kuwapora wengi haki yao.

Makene si unamkubuka Mchungaji sijui wa kanisa gani vile Mtikila, alilipigania mno suala la mgombea binafsi mpaka leo hajafanikiwa, badala yake walimwita kichaa.

Ndesanjo Macha said...

Naunga mkono kuondolewa takrima. Lakini naungana nawe kusema kuwa mabadiliko yanayotokewa kuboresha demokrasia na maisha ya watu yanahitaji kuendana na kubadili mitazamo, fikra, na muhimu kabisa mifumo ya utawala, uchaguzi, usajili wa vyama, na bila kusahau katiba.

jakogallo said...

mimi naingalia dhana nzima ya takrima lakini sioni kosa lake.kama kweli ni ahsante ya dhati.mzee wa mshitu hivi mtu akikusaidia ukapata kile ulichokitaka hupaswi kumshukuru??mi nasema namna invyotumika ndo mbaya lakini takrima bwana ni nzuri ila kama inutmika kukublackmail(utanisaidia hapo na kiswahili chake bw.makene)au kukudhulumu hapo hata mimi naipinga.halufu kinacho nishangaza ni kuwa ahsante hii ilikuwa kwenye katiba.hivi kutoa shukurani si hiari kwa nini iwe sheria.Jamani watanzaia sie.!!!anyway takrima kidhana mi naona ni nzuri na ikitumika vizuri itapunguza maovu mengi kama rushwa.kwa mfano mhudumu wa baa amekuhudumia vizuri hivi kumuachia buku hapo ni noma?lakini fanya hivyo unavyoondoka kwa maana shukuru baada ya huduma sasa hii ya wanasiasa wanafanya wakati wa kampeni hata hawajui kama watahinda hapo ndo swala lingine linaloniochanganya.ila mi nafikiri tuanzeni hiyo tabia kutoa shukurani baada ya kusaidiwa na pia iwe kwa vitendo jamani maneno matupu hayalambwi,mkaribishe daktari aliyekuhudumia vizuri hospitalini hata chakula cha jioni nyumabani kwako mle wali maharage pamoja kama njia ya ahsante,hata utume kadi basi au kapesa kadogo kama unako.lakini iwe baada ya huduma si kabla.