Thursday, May 29, 2025

BUNGE LAPITISHA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 164.1 SEKTA YA ARDHI





Bunge limepitisha na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kiasi cha shilingi 164,146,052,000/= ili kuendelea kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali nchini.

Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio na Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 jijini Dodoma leo tarehe 29 Mei 2025, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, wizara hiyo imejipanga kuwahudumia watanzania katika sekta ya ardhi ili kuwaletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla. 

Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, Wizara ya Ardhi inakusudia kuanzisha Kamisheni ya Ardhi ambayo itaweka mfumo mmoja wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi katika ngazi zote hatua aliyoieleza kuwa, itasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya sekta.

“Tumechelewa sana kuwa na Kamisheni ya Ardhi, tumechelewa sana kuhakikisha nchi yetu imepangwa na kupimwa. Kamisheni itasaidia uwajibikaji katika mamlaka zote katika shughuli za sekta ya ardhi zinatekelezwa katika ngazi ya Wizara, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa” amesema Waziri Ndejembi.

Aidha, Waziri Ndejembi ameweka wazi kuwa, ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, Wizara ya Ardhi imependekeza kuwepo Sheria ya Milki itakayoanzisha Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Milki (RERA).

Mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kuunda mfumo madhubuti wa usimamizi wa sekta ya milki, kuratibu na kutunza taarifa wadau na soko la milki, kusimamia tija na ufanisi wa wataalam wa sekta pamoja na kudhibiti uhalifu wa utakatishaji fedha haramu. 

“Natoa wito kwa wadau wote wa sekta ya milki kuhakikisha wanasajiliwa na kutambuliwa na Serikali ili kuimarisha ushirikiano na ukuaji endelevu wa sekta hii muhimu katika uchumi wa nchi” amesema Waziri Ndejembi. 

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa jimbo la Mtera mkoa wa Dodoma Mhe. Livinstone Lusinde ameitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kuwahudumia watanzania kwa kutenda haki ili kuacha alama kwa watu kupata haki zao. 

Wednesday, May 28, 2025

RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA MAKAO MAKUU YA CCM DODOMA


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiweka jiwe la msingi, kuashiria kuzindua rasmi kuanza kwa ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya CCM, katika hafla iliyofanyika eneo la Tambuka reli, jijini Dodoma, litakapojengwa jengo hilo. Uzinduzi huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi mbalimbali, wakiongozwa na viongozi na wanachama wa CCM, umefanyika leo Jumatano, tarehe 28 Mei 2025.












Dodoma, Mei 28, 2025

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya CCM, zitakazojengwa katika eneo la Tambuka Reli, jijini Dodoma.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakiwemo viongozi wa kitaifa, viongozi wa chama, wanachama wa CCM na wadau wengine wa maendeleo. Tukio hili linaashiria hatua kubwa katika kukamilisha dhamira ya chama ya kuwa na Makao Makuu yake katika Makao Makuu ya nchi, kama ilivyoasisiwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo la kisasa ni kielelezo cha uimara wa chama na dhamira ya kuendelea kuimarisha taasisi ya CCM katika nyanja za kiutawala, kihistoria na kimkakati.

"Leo tunaweka jiwe la msingi si tu kwa jengo, bali kwa historia ya chama chetu, ambacho kimekuwa chombo muhimu cha kuongoza maendeleo ya nchi hii kwa zaidi ya miaka 60. Dodoma kama Makao Makuu ya nchi, inastahili kuwa na Makao Makuu ya chama tawala yenye hadhi na mvuto wa kisasa," alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel John Nchimbi, alieleza kuwa jengo hilo litakuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia shughuli zote kuu za chama kwa ufanisi, na kwamba litajengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya ujenzi, mazingira na teknolojia.

Jengo hilo la Makao Makuu ya CCM linatarajiwa kuwa la ghorofa kadhaa, likijumuisha ofisi mbalimbali, kumbi za mikutano, sehemu za kumbukumbu za kihistoria za chama, na maeneo mengine muhimu kwa shughuli za ndani na za kimataifa za chama.

Ujenzi huu pia unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi katika jiji la Dodoma, kuongeza ajira na kuboresha miundombinu ya mkoa huo unaoendelea kukua kwa kasi kama kitovu cha utawala wa Tanzania.

Hafla ya leo imeacha alama ya kihistoria na kuonesha mshikamano mkubwa miongoni mwa wanachama na wapenzi wa chama hicho, huku ikibeba ujumbe wa matumaini na maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKUTANA NA VIONGOZI WA WIZARA YA ARDHI YA JAPAN NA SHIRIKISHO LA WAWEKEZAJI (JAIDA)





Tokyo, Japan – Mei 27, 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan, Mheshimiwa Hiromasa Nakano, katika Makao Makuu ya Wizara hiyo jijini Tokyo, Japan.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan hususan katika maeneo ya ardhi, miundombinu na usafirishaji. Viongozi hao walijadili njia za kuendeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Miundombinu la Japan (Japan Infrastructure Development Association – JAIDA), Bw. Miyamoto Yoichi, pamoja na ujumbe wake.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuhamasisha wawekezaji wa Japan kuwekeza Tanzania, hususan katika sekta za ardhi, miundombinu na usafirishaji. Waziri Mkuu aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na sera thabiti, usalama wa mitaji, na fursa lukuki zinazopatikana kupitia programu na miradi ya kimkakati ya serikali.

Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka Japan katika kuendeleza miradi ya kielelezo yenye lengo la kuchochea maendeleo ya taifa, na kutoa ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wao, viongozi wa JAIDA walionesha nia ya dhati ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwekeza kwenye miradi yenye tija, huku wakivutiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.

Mwisho wa ziara hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwashukuru viongozi wa Serikali ya Japan na wadau wa sekta binafsi kwa ushirikiano wao na kuahidi kuendeleza mazungumzo hayo kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili.

Tuesday, May 27, 2025

TANZANIA NA KOREA KUSINI ZAENDELEZA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA KATIKA SEKTA YA ARDHI NA MAKAZI

 














 




Dodoma, Mei 27, 2025 — Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo ya kikazi na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Uchukuzi wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Bw. Jin Hyun Hwan, katika kikao maalum kilichoandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mkutano huo umefanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) –  Mkandarasi House Dodoma, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa NHC alikuwa mwenyeji kwa niaba ya wizara, akiwapokea viongozi hao waandamizi na kuwakaribisha katika jengo hilo la kihistoria.

Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili kwa kina njia za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati baina ya Tanzania na Korea Kusini, hasa katika maeneo ya usimamizi wa ardhi, uendelezaji wa makazi nafuu, na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika upangaji wa miji na utunzaji wa mazingira.

Waziri Ndejembi alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora na nafuu kwa wananchi, akieleza hatua zinazochukuliwa kupitia miradi kama Samia Housing Scheme, pamoja na mapendekezo ya kushirikiana na Korea katika uboreshaji wa mifumo ya kidijitali ya taarifa za ardhi.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Jin Hyun Hwan alitoa pongezi kwa juhudi za Serikali ya Tanzania na kueleza kuwa Jamhuri ya Korea iko tayari kuendeleza ushirikiano kupitia:

    Mradi wa National Land Data Infrastructure (NLDI) unaolenga kuboresha taarifa za kijiografia na ramani za kitaifa;

    Uendelezaji wa Tanzania Geo-Innovation Center, kituo cha mafunzo ya teknolojia ya ardhi na upimaji kwa kutumia droni na GIS, kinachotarajiwa kuanza rasmi Julai 2025;

    Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wataalamu wa Kitanzania kupitia ushirikiano wa kitaaluma na programu za Knowledge Sharing Program (KSP);

    Uboreshaji wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi vya kisasa na rafiki kwa mazingira, kama vile mifumo ya kiyoyozi na vifaa vya ujenzi vinavyotumika nchini Korea.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea Kusini ulioanzishwa mwaka 1992 umeendelea kuimarika kwa miaka, na mkutano huu ni ushahidi wa dhamira ya pamoja kuendeleza maendeleo jumuishi na endelevu yanayozingatia matumizi bora ya ardhi, makazi bora, na teknolojia rafiki kwa mazingira.

Monday, May 26, 2025

Nipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi kufikia malengo ya Mhe. Rais – Prof. Tumaini Nagu








Na. OR – TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya Prof. Tumaini Nagu amefanyiwa mapokezi makubwa na viongozi, menejimenti na watumishi wa ofisi hiyo ambapo ameahidi ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali.

Prof. Nagu ameyasema hayo wakati akiongea na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru, baadhi ya viongozi, menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI baada ya mapokezi yake katika ofisi za Wizara zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kuomba ushirikiano na kuahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia dhamira na maono ya Mheshimiwa  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini na kumteua ili aisimamie Sekta ya Afya hususani Afya ya msingi chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na amepokea kwa unyenyekevu mkubwa uteuzi wake na kuahidi kushirikiana kwa vitendo lakini anaamini uzoefu huongezeka kila siku na yupo tayari kufanya kazi na viongozi na watumishi wa ofisi hiyo.

Prof. Nagu afafanua kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maelekezo yake kwa kusisitiza kuboresha huduma za afya ya msingi, huduma ambazo zinatakiwa kuwafikia wananchi kwa wakati na dhamira yake ni kuyafanya mazingira ya afya kuwa bora, hivyo kama sehemu ya ofisi ambayo anakutana na wazoefu watamsaidia na kushirikiana naye ili kuyafanya hayo kwa vitendokwani kidole kimoja hakivunji chawa.

“lakini naomba itoshe sana kusema nakushukuru Katibu Mkuu (Bw. Adolf Ndunguru) pamoja nanyi nyote ambao mmenipokea siku ya leo, na hii ni ‘surprise’ kubwa, ishara kubwa kwamba mpo tayari kushirikiana nami na hilo ndilo ninaloliomba, tushirikiane ili tuweze kuwatumikia watanzania na yale maono ya Mheshimiwa Rais, basi yakatekelezeke kwa kumuunga mkono Rais wetu” alilisisitiza Prof. Tumaini Nagu 

Katibu Mkuu Adolf Ndunguru Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru amemkabidhi Kiongozi huyo Mpango Mkakati wa Taasisi na Muundo wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusesema kuwa anamjua Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Prof. Tumaini Nagu kama mtu mzoefu katika Sekta ya Afya na anaamini kuwa atafanya kazi nzuri na kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI yenye Idara na Vitengo 17 imempokea na itakuwa tayari kupokea maagizo yake na kuyafanyia kazi ili kuweza kufikia malengo na maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.   

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Emma Lyimo akitoa neno kabla ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru katika kikao kifupi cha menejimenti kumkaribisha Prof. Tumaini Nagu, amesema anayo furaha kubwa ya Kiongozi huyo mahiri kujiunga na familia ya Ofisi ya Rais TAMISEMI lakini pia kupata wasaa wa kukutana na kufahamiana na Viongozi, menejimenti na watumishi Ofisi ya Rais TAMISEMI.

MAPEPELE AWANOA MAAFISA HABARI WA TAMISEMI, AWATAKA WAWE WAZALENDO





Na Mwandishi Wetu, OR- TAMISEMI

Mkuu wa Kitengo Cha Mawasilino Serikali na Msemaji wa Wizara ya TAMISEMI, John Mapepele ametoa wito kwa Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kutanguliza uzalendo na weledi wakati wa utoaji wa taarifa ili habari hizo ziwe na tija kwa taifa.

Mapepele ametoa wito huo mwisho wa juma  wakati akiwasilisha maada kuhusu Mawasilino ya Kimkakati ya Kutangaza Nafanikio ya Sekta za Afya, Elimu na Miundombinu chini ya TAMISEMI kwa Maafisa Habari  zaidi ya 200 wa Mikoa na Halmashauri zote nchini jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha siku mbili kwa MaafisaHabari hao kilichoratibiwa na Wizara hiyo.

Kikao kazi hicho kilichofunguliwa  na  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe.Mohamed Omary Mchengerwa na kufungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa kimejadili pamoja na mambo mengine, mikakati mbalimbali ya kutangaza mafanikio ya Serikali, pia kuwajengea uwezo Maafisa Habari hao kwa mada mbalimbali za kitaaluma hususan matumuzi ya mifumo ya kidigitali kwenye utoaji wa taarifa na kuja na maazimio kadhaa ya kuboresha utendaji kazi.

Aidha, Mapepele amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika mikoa na Halmashauri zote nchini ambayo haijatangazwa ipasavyo na Maafisa Habari katika maeneo hayo  na kuwataka kuwa wabunifu wa kutoa taarifa hizo

"Ndugu zangu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa kwenye  sekta ya miundombinu ambapo tumeshuhudia mabarabara, madaraja, vituo vya mabasi na masoko yakitengenezwa kila uchao, ukiachia mbali madarasa, zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba kwenye kila kona hivyo ni wajibu wetu sisi Maafisa Habari wa Halmashauri na Mikoa kuwa wazalendo na kuisemea Serikali yetu ili wananchi waweze kujua na kutumia huduma hizi kikamilifu". Amefafanua Mapepele 

Akifungua kikao kazi hicho Mhe. Mchengerwa amewataka  Maafisa Habari wote wa TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi kwa wakati za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa  na Serikali katika maeneo yao ya kazi.

"Mmebeba dhamana kubwa  ya kuhakikisha  wananchi wanapata  habari sahihi hivyo msiache watanzania walishwe habari potofu". Amesisitiza Mhe. waziri Mchengerwa 

Akifunga kikao kazi hicho, Katibu Mkuu Msigwa ameipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kuratibu kikao kazi hiki ambapo ameshauri  kiwe kinafanyika kila mwaka ili kufanya tathmini wa utendaji wa kazi na kujadiliana masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi wa kundi hili kubwa la Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri nchini katika kutoa taarifa za miradi ya maendeleo.

Mara baada ya kumalizika  kikao kazi hiki, Maafisa Habari hao walipata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali wa Mtumba na kujionea kukamilika kwa Mji huo

PPAA yatoa rai wazabuni kutumia moduli kuwasilisha rufaa

  Na Mwandishi wetu, Dar Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa rai kwa wazabuni kutumia Moduli ya kupokea na kushughulikia malal...