Dar es Salaam, 22 Januari 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili jijini Dar es Salaam leo kwa usafiri wa treni ya umeme ya Reli ya Kisasa (SGR) akitokea mkoani Dodoma.
Safari hii ya kihistoria inadhihirisha dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia ya kuboresha miundombinu ya usafiri wa reli ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Rais Samia alipowasili katika stesheni ya Dar es Salaam, alipokelewa na viongozi waandamizi wa serikali, wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa, na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili la kihistoria.
Rais Samia amesifu maendeleo ya mradi wa SGR na kusisitiza umuhimu wake katika kupunguza gharama za usafirishaji wa abiria na mizigo, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, na kuimarisha mahusiano ya kibiashara ndani na nje ya nchi.
Mradi wa SGR umeendelea kuwa moja ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Tanzania, ukiwa na lengo la kuunganisha nchi na kukuza uchumi wa kikanda. Treni hii ya kisasa inatarajiwa kuboresha viwango vya usafiri salama, wa haraka, na wa kuaminika kwa Watanzania na wageni.
Tukio hili limeonyesha tena mafanikio ya jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo kwa maslahi ya taifa.
No comments:
Post a Comment